Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe amekosoa uamuzi wa mwenyekiti wa chama cha Wananchi (CUF) anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuhusu mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho.

Rungwe ambaye alikuwa miongoni mwa wagombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana amesema kuwa kutokana na alichokifanya Profesa Lipumba muda mfupi kabla ya kampeni za mwaka jana anapaswa kuwaomba radhi wa Watanzania na wafuasi wa chama chake.

 

“Profesa Lipumba anatakiwa akubali kuwa alifanya maamuzi kwa pupa na alitumia zaidi uprofesa badala ya busara. Anatakiwa awaombe radhi wafuasi wa chama hicho na Watanzania kwa uamuzi wake wa awali,” Rungwe anakaririwa na Mwananchi kupitia mahojiano aliyofanya hivi karibuni.

Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu nafasi yake ya Uenyekiti Agosti mwaka jana, muda mfupi baada ya chama chake na yeye mwenyewe kutangaza kumuunga mkono mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa kupitia Ukawa.

Lipumba alirejea tena mwaka huu na kutangaza kutengua uamuzi wake huku Baraza Kuu la chama hicho nalo likitangaza kumvua uanachama. Kutokana na sakata hilo, msomi huyo aliandika barua ya malalamiko kwa Msajili wa Vyama vya Siasa iliyozaa matunda kwa upande wake baada ya kutambuliwa rasmi na ofisi hiyo.

Baraza Kuu la CUF lilifungua kesi Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Msajili ikiiomba mahakama kubatilisha barua hiyo na kuamuru Msajili kutoingilia maamuzi ya chama.

Obama afunguka kuhusu mpango wa Mkewe kugombea Urais Marekani
Nape awachambua wanaobeza uwekezaji