Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amejibu matokeo ya utafiti uliofanywa unaoonesha kuwa anatajwa na asilimia 33 ya Wakenya kuwa anaongoza kwa vitendo vya rushwa.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi ya Ipsos Synovate, iliyopitia Kaunti 45 na kuwahoji jumla ya watu 2,000 unamuweka Ruto kwenye nafasi ya kwanza akiwa na silimia 33, akifuatiwa na Gavana wa Kirinyaga ambaye amepata asilimia 31.

Kadhalika, utafiti huo umeonesha kuwa asimilia 51 ya Wakenya wana imani na jinsi ambavyo Rais Uhuru Kenyatta anapambana na vitendo vya rushwa.

Ruto ameeleza kuwa utafiti huo umefanywa kama propaganda ya kumchafua kwakuwa wapinzani wake hawawezi kushindana naye kwenye rekodi ya kuwaletea maendeleo Wakenya.

“Wakimalizana na propaganda zao za vichwa vya habari, tukutane kwenye kilinge cha kuwaletea maendeleo Wakenya kwa sababu hapo ndipo ushindani wa kweli  ulipo,” alisema Ruto.

“Wapinzani wangu wakimalizana na utafiti walioufadhili, habari za uongo, tukutane kwenye hiki kilinge cha kuleta maendeleo kinachomlenga mwananchi wa chini, reli ya kisasa, pato la mwananchi, barabara, kuwaunganishia wananchi umeme, kuboresha huduma za afya na mani. Nawangojea huko,” aliongeza.

Utafiti huo unachukuliwa na wafuasi wa Ruto kama njia ya kutaka kukwamisha mbio zake za kuelekea Ikulu, kwani imewekwa wazi kuwa atawania nafasi ya urais katika uchaguzi ujao wa mwaka 2022.

Hata hivyo, utafiti wa Ipsos haukuwaacha salama wanasiasa wengine, Daniel Arap Moi (Rais Mstaafu), Mwai Kibaki (Rais mstaafu), Raila Odinga (Kiongozi wa upinzani) na Rais Kenyatta wametajwa kwenye nafasi sita za juu japo wana asilimia chache.

 

NACTE yatoa ufafanuzi ucheleweshaji wa namba ya uhakiki AVN
Utafiti: Njugu zinavyoboresha nguvu za kiume