Gwiji wa soka kutoka nchini Uholanzi, Ruud Gullit amesema yupo tayari kukinoa kikosi cha Aston Villa, licha ya kukabiliwa na mtihani wa kuwa katika janga la kushuka daraja.

Gullit amesema pamoja na kuifananisha kazi hiyo sawa na kukubali kubeba gunia la misuri, lakini anaamini kwake inawezekana, kufuatia uzoefu mkubwa alionao wa kupambana na kufanikisha azma ya kushinda.

Gullit ambaye aliwahi kuvinoa vikosi cha Chelsea pamoja na Newcastle Utd kama meneja, amekubali jambo hilo alipozungumza na kituo cha televisheni cha beIN Sport baada ya kuulizwa nini muono wake katika mustakabali wa klabu ya Aston Villa ambayo imedumu kwa muda mrefu kwenye ligi kuu ya soka nchini England.

Gwiji huyo amesema ni masikitiko makubwa sana kwake pamoja na kwa wadau wengine wa soka duniani, kuona Aston Villa ipofika kwa sasa, lakini hakuna budi kwa viongozi kusaka mbinu mbadala kunusuru hali iliopo.

Amesema anatambua kwa sasa viongozi wa The Villians wanasaka meneja aliye sahihi katika mtihani unaowakabili lakini kama atafuatwa na kuombwa aifanye kazi hiyo hatokua na hiyana yoyote.

Hata hivyo Gullit mwenye umri wa miaka 53 amekua nje ya ukufunzi tangu mwaka 2011, alipofukuzwa kwenye klabu ya Terek Grozny ya nchini Urusi.

Aston Villa walifikia maamuzi ya kuachana na meneja kutoka nchini Ufaransa Remi Garde, usiku wa kuamkia jana baada ya kuchoshwa na huduma zake za ukufunzi ambazo zilishindwa kuleta tija ya ushindani klabuni hapo.

Aston Villa inaendelea kuburuza mkia katika msimamo wa ligi kuu ya soka nchini England kwa kumiliki point 16 zilizotokana na ushindi wa michezo mitatu, sare saba na kupoteza ishirini na moja.

Emmanuel Eboue Afungiwa Kucheza Soka
Viongozi Wa Stand Utd Waufyata Kwa Patrick Liewig