Maafande wa Ruvu Shooting wametamba kuibuka na ushindi katika mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Kinondoni Municipal Council (KMC FC), Jumamosi wiki hii.

Tambo za maafande hao kutoka Mlandizi mkoani Pwani, zimekuja baada ya kuwabana mabingwa watetezi Simba SC kwenye mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita Uwanja wa Taifa Dar es salaam, na kumbaulia alama moja, kufuatia matokeo ya bao moja kwa moja.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema, wachezaji wao wako tayari kwa mapambano ya michezo ijayo, baada ya kumalizana na Simba, hivyo amewataka KMC wakae mkao wa kula.

Amesema Ruvu Shooting haitokuwa na mzaha katika mchezo wa Jumamosi dhidi ya KMC, huku akiwataka Kino Boys wajitayarishe kufungwa mabao mawili.

“Ya Simba yamepita, sasa hivi ni zamu ya hao wanaojiita watoto wa Kinondoni sasa wajiandae kuchapika hao majirani zao waliponea chupu chupu,” alisema Masau.

Masau amesema kwa sasa vijana wao wako vizuri na wanaendelea na maandalizi ya kutosha kuhakikisha wanaibuka na kuchukua alama tatu katika mchezo huo.

Ruvu Shooting kwa sasa inashika nafasi ya 11 ikiwa na alama 40 huku KMC ikishika nafasi ya 15 ikiwa na alama 33.

Tetesi: Leicester City, Crystal Palace zamuwania Tarkowski
Ndalichako ataja ratiba ya mitihani, "Wazazi wavumiliwe ada"