Kwa heri Ibrahim Akilimali

Daima tutakukumbuka

Uongozi wa Ruvu Shooting Star, umepokea kwa masikitiko, simanzi na majonzi makubwa, taarifa za msiba wa mzee Ibrahim Akilimali, mmoja wa wazee kakini, mahiri, mkweli na muwazi katika maendeleo ya soka la Tanzania akiwaongoza wazee wa klabu ya Young Africans, aliyefariki alfajiri December 14, 2019, nyumbani kwake, Mapinga, Bagamoyo.

Taifa limeondokewa na mtu muhimu sana katika sekta ya michezo, hususani soka, Klabu ya Young Africans imempoteza mzee ambaye kwa kweli, sisi Ruvu Shooting tulimuona kama jicho la marekebisho, matengenezo na mafanikio kwa klabu hiyo kongwe, yenye masikani yake, mitaa ya Jangwani, Dar Es salaam.

Ruvu Shooting tunaamini, kifo cha mzee Akilimali, kimewashutua Watanzania wapenda soka, kwa namna ambavyo walishibishwa na hoja zenye nguvu za hoja kutoka kwake, zaidi sana, Wanahabari kwa ujumla wao, wamempoteza mtu muhimu sana, aliyekuwa akiwapa ushirikiano mkubwa sana katika kazi yao, alikuwa chanzo kizuri mno cha habari, hasa zilizoihusu klabu yake ya Young Africans.

Mzee Akilimali aliupenda mpira wa miguu, aliipenda sana klabu yake, alikuwa tayari kuusema ukweli bila kujali atamfurahisha au kumkera nani lakini ahakikishe klabu yake ya Young Africans inafikia mafanikio, hakika tumepoteza jabari la soka Tanzania!

Poleni Young Africans,  poleni Watanzania kwa msiba huu, Ruvu Shooting, tupo pamoja katika maombolezo ya msiba wa mzee wetu.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa,  Jina lake lihimidiwe…..

Nenda Akilimali, daima tutakukumbuka, ulifanya uliyopaswa kufanya katika soka la Tanzania, kwa moyo na mafanikio makubwa, hukuwa mnafiki,  ulikuwa mkweli na muwazi, watu wa aina yako ni wachache, wengi wanaangalia zaidi matumbo yao na hujipendekeza matumbo yao yashibe na kuogopa kusema ukweli, wakiofia kuchukiwa kwa ukweli wao ambao ndio ukweli, tabia ambayo kwako haikupata nafasi…

 

Masau Kuliga Bwire

Afisa Habari Ruvu Shooting.

Mfungwa aliyeachiwa kwa msamaha auawa na wananchi, baada ya kuwachoma watu visu na kuua.
Zanzibar: Daktari kizimbani kwa kuomba rushwa ya ngono kwa Mjamzito