Meneja wa Mabingwa wa soka Tanzania Bara Simba SC, Patrick Rweyemamu, amesema wachezaji wa timu hiyo wapo katika hali nzuri, baada ya kuwapa mapumziko ya siku moja.

Simba SC wameanza maandalizi ya kuelekea mpambano huo, baada ya kurejea jijini Dar es salaam juzi Jumatatu, walikocheza mchezo wa mzunguuko wa kwanza dhidi ya Ihefu FC ambao walikubali kichapo cha mabao mawili kwa moja.

Mbali na kuanza mazoezi jana Jumanne, kikosi cha Mabingwa hao kimeanza rasmi kambi hii leo jijini humo, kabla ya kuanza safari ya kuelekea mkoani Morogoro tayari kwa kuwakabili Mtibwa Sugar, katika matanange wa mzunguuko wa pili Septemba 13.

“Tunashukuru mchezo ulimalizika salama, hakuna majeruhi kwa sasa wachezaji wameelekeza mawazo na akili kwenye mchezo wetu unaofuata ambao tutacheza Morogoro dhidi ya Mtibwa Sugar,” amesema Rweyemamu.

Ameongeza wamejipanga kukabiliana na changamoto katika mchezo huo kwa sababu wanafahamu wenyeji wao ni moja ya timu zinazotoa upinzani kila wanapokutana.

“Tumejipanga na tunaamini wao (Mtibwa), pia wamejiandaa, tutaingia kwa kasi kwa sababu tunahitaji ushindi, ndio malengo yetu,” Rweyemamu amesema.

Pia ameeleza kuwa wachezaji wao watatu ambao ni Paschal Wawa, Luis Miquisson na Larry Bwalya waliokosekana katika mchezo dhidi ya Ihefu FC wameungana na wenzao na wanaamini wataongeza nguvu katika kikosi hicho cha Wekundu wa Msimbazi.

Watanzania msisafiri bila vibali - RC Mtwara
Baraza atoa kongole Biashara United Mara