Wachezaji Saba wa Young Africans waliokua kwenye Kikosi cha Taifa Stars wamejiunga na wenzao Kambini Avic Town, tayari kwa Maandalizi ya Msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.

Wachezaji Feisal Salum ‘Fei Toto’, Abutwalib Msheri, Kibwana Shomari, Farid Mussa Malik, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ waliitwa Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN’ dhidi ya Somalia.

Wachezaji hao walianza mazoezi sambamba na wenzao wa Young Africans jana Jumatatu (Agosti 02), na kukifanya kikosi cha klabu hiyo kukamilika Rasmi, baada ya kuanza na wachezaji wachache ambao hawakuitwa kwenye timu zao za taifa.

Beki Dickson Job amesema amefurahia kujiunga na wachezaji wenzake wa Young Africans kwa mara ya kwanza baada ya kumaliza msimu uliopita (2021/22), ambapo walipata mafanikio makubwa kwa kutwaa Ubingwa wa Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Ngao ya Jamii.

Amesema ameshuhudia ushindani mkubwa katika mazoezi ya kikosi cha Young Africans kufuatia usajili wa wachezaji wengine wa kigeni, hivyo anatarajia kuona kikosi chao kikiwa bora zaidi msimu ujao, ambao utaanza rasmi juma lijalo.

“Nimefurahi kuwa sehemu ya kambi ya timu yangu, hii ni mara ya kwanza katika kipindi hiki baada ya kumaliza msimu uliopita kwa mafanikio makubwa, nimeona ushindani umeongezea na hali hii itaendelea kuleta ubora katika kikosi chetu.”

“Lengo kuu hapa ni kuipigania Young Africans, sitegemei wala kusikia tofauti baina ya mchezaji na mchezaji kwa kisingizio cha kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza, wote lengo letu ni kuiwezesha timu yetu kuwa bora na kutetea mataji yake msimu ujao.” amesema Job

Naye Nahodha na Beki Bakari Nondo Mwamnyeto amekiri uwepo wa ushindani katika maandalizi ya kikosi chao, huku kila mchezaji akiwania nafasi ya kupenya katika kikosi cha kwanza.

“Kweli ushindani upo, umeongezeka tofauti na msimu uliopita, nimeona katika siku yangu ya kwanza baada ya kujiunga na wenzangu hapa AVIC Town, kwa hakika tutakuwa na timu bora sana kwa msimu ujao.” amesema Bakari

Young Africans itaanza kucheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki katika hadhira siku ya Wananchi, Jumamosi (Agosti 06) baada ya kucheza michezo ya kirafiki kambini juma lililopita dhidi ya Friends Rangers na Trans Camp.

Agosti 13 Young Africans itatetea Ngao ya Jamii kwa kucheza dhidi ya Simba SC, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Bei ya mafuta nchini yazidi kupaa
Makinda: Sensa siyo zoezi la siku moja