Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani ya mwili Dk. Meshack Shimwela amesema zipo sababu tofauti zinazosababisha vifo vya ghafla, baadhi ikiwa ni maradhi ya moyo, mapafu, ubongo, mfumo wa upumuaji na wakati mwingine sumu.

Dk. Shimwela amesema uginjwa wa moyo unasababisha vifo kwa asilimia kubwa kwa sababu mishipa au milango ya moyo  inaweza kupasuka; athari za dawa kwenye moyo; moyo kukosa hewa safi au kiungo kimoja kukosa usambazaji wa damu.

“Tatizo la Watanzania wengi ni kuwa hatuchunguzi afya zetu mara kwa mara. Watu wengi wanatembea na maradhi bila kufahamu na hicho ndicho chanzo cha vifo vya ghafla,” anasema Dk. Shimwela

Anasema inawezekana kabisa kuwa mtu aliyefariki ghafla  alikuwa akiugua kwa muda mrefu bila kuchukua tahadhari au kudharau hali yake na wakati mwingine alikuwa akiumwa lakini hakufuata masharti ya ugonjwa wake.

“Kikubwa baada ya vifo vya ghafla ni kufanya uchunguzi wa sababu ya kifo hicho (postmortem)  badala ya kuhisi tu,” anasema

Mara nyingi sababu kuu huwa ni matatizo katika mishipa inayopeleka damu katika  misuli ya moyo mishipa hiyo huathirika kutokana na urundikaji wa lehemu mwilini hivyo kusababisha mishipa hiyo kunyauka na kukakamaa hivyo kuifanya ishindwe kutanuka na kuwa myembamba.

Urundikaji wa lehemu  katika mishipa hii pia husababisha kutokea kwa vichuguu katika mishipa midogo inapeleka damu katika moyo hivyo kuwa kama kizuizi cha damu kupita.

Vilevile, damu iliyoganda nakuwa kama vibuja vya ugali huweza kutoka sehemu yoyote ya mwili kupitia mzunguko wa damu hufika katika mishipa inayopeleka damu safi katika misuli ya moyo na kuwa kizuizi cha damu kupita, hivyo basi mambo haya matatu yakitokea husababisha misuli ya moyo kukosa damu kabisa ua kupata kiasi kidogo sana.

Dk. Jennifer Ndosi, bingwa wa magonjwa ya ndani wa Hospitali ya Mount Meru, Arusha anasema misuli ya moyo ikikosa damu, huharibika na kushindwa kufanya kazi ya kusukuma damu kwa ufanisi wa kawaida.

Misuli ya moyo huharibika na kuifanya misuli ya moyo kupiga bila mpangilio na ndipo ghafla moyo husimama kudunda.

Anaeleza kuwa sababu ya pili ni misuli ya chumba cha upande wa kushoto wa moyo kuongezeka ukubwa na mara nyingi huwapata wenye shinikizo la damu la muda mrefu hii ni kutokana na kujibadili kwa misuli ya moyo na kuongezeka ukubwa na kufanya kazi ya ziada ya kusukuma damu.

Kuongezeka huku kwa misuli ya moyo husababisha vyumba vya moyo kuwa na nafasi ndogo ya kupokea damu na pia kushindwa kusukuma vizuri damu.

Sababu nyingine ni ya magonjwa mengine ya moyo ni kama vile moyo kushindwa kufanya kazi, maumbile yasiyo ya kawaida ya mishipa ya damu, uambukizi wa valvu za moyo na hivyo valvu kushindwa kufanya kazi.

Nyingine ni  matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo, matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo, usafirishaji taarifa katika moyo, upungufu wa madini kama vile magnesium, kuzaliwa na moyo mkubwa, kuwa na wingi wa mafuta mabaya mwilini.

Mambo mengine ambayo hayatokani na maradhi ya moyo yanayoweza kuwa chanzo cha vifo vya ghafla ni sumu, au mrundikano wa taka mwili  zenye sumu, matatizo ya mfumo wa hewa, kupaliwa na kitu katika mfumo wa hewa, kuvuta hewa chafu na ajali.

Pia, hali ya kifo hiki huweza kutokea na sababu isijulikane.

Flaviana Matata atokea kwenye tangazo la Rihanna
Watendaji sekta ya uchukuzi watakiwa kufanyakazi kwa weledi