Watu 110 wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) waliokuwa wameanza kutumia dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo (ARVs) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), wameacha kutumia dawa hizo kutokana na sababu mbambali  na 5% kati yao ni vijana wenye umri kati ya miaka 16 hadi 24.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Maambukizi ya MNH, Amina Mgunya amesema wapo walioacha kutumia dawa hizo kwa madai ya kuwa wameokoka na kuhudhuria maombi kanisani, wengine wameacha kwa kuwa na imani potofu na kukimbilia kwa waganga wa kienyeji, lakini pia wapo walioacha kuhudhuria kliniki kwa madai kuwa wanaogopa wenzi wao.

“Wanahofia kwamba itakuwaje siku watakapogundua kuwa wanahudhuria kliniki hiyo na wanatumia dawa hizo. Kuna hofu ya kunyanyapaliwa, huwa wanapatiwa kadi maalum ya kuchukua dawa hizo, hapa hospitalini huwa wanachukua dawa katika dirisha moja na wagonjwa wengine,” amesema Mgunya.

Amesema tangu 2004 hadi sasa wagonjwa 10,047 wamehudumiwa katika kliniki hiyo, kati yao wanawake ni  6,282 na wanaume ni 3,765 na kwamba wagonjwa 346 wamefariki dunia na 4,971 wamehama (wamehakikishwa) kituo.

“Muhimbili ni hospitali kubwa inayopokea wagonjwa wa rufaa kutoka katika maeneo mbalimbali nchini, mtu anapopewa rufaa kuja huku na kulazwa, tukimpima  na kukutwa ana maambukizi, tunamuanzishia dawa papo hapo, hii ni kulingana na mwongozo wa sasa wa serikali.

“Huwa tunawapa kadi maalum (blue card) ambayo huwa na namba maalum ya usajili wake, kadi hiyo huitumia kupata huduma ikiwamo dawa za ARVs kliniki na ikiwa ataruhusiwa kurejea nyumbani, ataendelea kupata huduma kwenye hospitali yoyote kwa kutumia kadi hiyo hata kama ni nje ya mkoa, Lakini ili kuwaondolea adha ya kuja Muhimbili mara kwa mara wagonjwa 4,971 wamehamishwa vituo vya karibu na maeneo yao,” alisema Amina.

Aidha Dk. Amina amesema kuwa wamebaini sababu nyingi zinazochangia watu wengi kuacha kutumia dawa za kupiunguza makali ya maambukizi ya Ukimwi ni hali kujinyanyapaa wenyewe, na katika kuliweka hilo sawa wagonjwa wote wa VVU pamoja na wagonjwa wa kawaida huchukua dawa katika dirisha moja.

Sakata la Mtawa kujiua laibua sura mpya, Kamanda atoa ufafanuzi
Liverpool kuangukia kundi la kifo?