Kuchelewa kupima ugonjwa wa kifua kikuu (TB) na matibabu kutowafikia wagonjwa wengi vimetajwa kuwa changamoto inayokabili juhudi za kutokomeza ugonjwa huo, hali inayoifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zenye kiwango cha juu cha wagonjwa duniani.

Hayo yameelezwa jana katika mkutano wa kufunga program ya kutokomeza TB iliyokuwa inaendeshwa na taasisi ya KNCV Tuberculosis Foundation, iliyokuwa inaitwa ‘Challenge TB’.

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile aliyehudhuria mkutano huo alisema kuwa TB bado ni changamoto nchini na akawataka wadau kushirikiana na wananchi katika vita dhidi ya ugonjwa huo. Alisema kuwa bila ushirikiano ambao umekuwa ukioneshwa hali ingekuwa mbaya zaidi.

“Mbali na changamoto, tumeona mafanikio katika hatua tulizochukua ikiwa ni pamoja na kuanzishwa kwa vituo vya matibabu ambavyo vimepunguza muda wa kuchukuliwa vipimo na matibabu kutoka siku tatu hadi saa kadhaa,” alisema Dkt. Ndugulile.

Aliongeza kuwa Serikali imejenga vituo vingi vya afya vinavyoshughulika na TB ili kuhakikisha kuwa watu wengi zaidi wanafikiwa.

Dkt. Ndugulile alieleza kuwa wadau wanapaswa kuhakikisha program zao zinaendana na sera na mipango ya Serikali ili wote wajikite katika njia moja ya kutokomeza ugonjwa huo.

Naye Naibu Mkurugenzi wa KNCV, Dkt. William Mbawala alisema kuwa kupitia program hiyo, asilimia 46 ya watu waliobainika kuwa na TB walipatiwa matibabu.

Dkt. Mbawala alisema kuwa TB iliyokomaa ni mzigo kwa Serikali kwani matibabu yake hugharimu zaidi.

Kwa mujibu wa takrimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna wagonjwa 150 wapya wa TB kila mwaka nchini.

Ufaransa yavunja rekodi ya kiwango cha joto, chafika nyuzi joto 45.9
Serikali inatambua na kuvithamini vituo vya kukuzia vipaji- Dkt. Mwakyembe