Cristiano Ronaldo amefunga mabao 58 miaka miwili iliyopita na kuwasaidia Real Madrid kushinda Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya mara mbili mtawalia na pia La Liga mara moja.

Miaka hiyo miwili iliyopita, ameshinda tuzo ya mchezaji bora duniani, tuzo ya Ballon D’Or, mtawalia. Anafaa basi kuwa mchezaji bora zaidi duniani na thamani yake kuwa ya juu zaidi?

Ni kweli uchezaji wake hauna kifani. Lakini kwa thamani, la hasha.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika la takwimu za michezo la CIES iliyotolewa Jumatano, mchezaji huyo ni wa 49 kwa thamani duniani.

Anayeongoza orodha hiyo ni mshambuliaji wa Paris St-Germain ya Ufaransa, Mbrazil Neymar, ambaye ndiye mchezaji aliyenunuliwa pesa nyingi zaidi na klabu yoyote duniani na mwenzake wa Barcelona Lionel Messi, kutoka Argentina.

Mshambuliaji wa Tottenham Harry Kane ameorodheshwa kuwa wa tatu. Unaweza kushangaa ni kwa nini thamani ya Ronaldo imekadiriwa kuwa $96,6 milioni.

Lakini tutajaribu kufafanua ni kwa nini watafiti wa CIES walifikia uamuzi huo ambao kwa wengi unaonekana wa kushangaza.

Tathmini ya thamani ya mchezaji sokoni huzingatia mambo mengi. Moja muhimu ni umri.

Ronaldo anakaribia kugonga miaka 33. Ronaldo si mzee wa kustaafu lakini anafikia ukingoni wa maisha yake ya uchezaji.

Kwa mujibu wa Chama cha Wachezaji wa Soka ya Kulipwa England kwa mfano, umri wa kawaida wa wachezaji kustaafu huwa miaka 35.

Wachezaji walio na umri wa juu kimsingi huumia zaidi, na wanapoumia, huchukua muda mrefu kupona.

Hili ni jambo ambalo klabu huzingatia zinapomnunua mchezaji.

“Sijaelewa ni kwa nini watu wengi hivi wameshangaa,” anasema Dkt Raffaele Polli, mmoja wa watafiti wanaoongoza katika CIES ameambia BBC.

“Ronaldo ni jina kubwa katika soka na mchezaji mzuri sana, lakini anakaribia kutimiza miaka 33 na miezi ya karibuni kiwango chake cha soka kimeanza kushuka. Wachezaji wachanga mara nyingi thamani yao huwa juu.

“Kusema kweli, thamani yake kwa mchezaji wa umri wake ni ya juu.”

Kuna uwezekano mdogo sana kwamba Paris Saint-Germain wangetoat $263m kumnunua Neymar Agosti iwapo mchezaji huyo angekuwa na umri zaidi ya umri wake wa sasa, miaka 25.

Kwa kweli, ni wachezaji wanne pekee wa zaidi ya miaka 29 ambao wamo orodha hiyo ya 100 bora, na Ronaldo ndiye ana umri wa juu zaidi.

Wengine ni Messi, Luís Suarez (Barcelona) na Gonzalo Higuaín (Juventus).

Lionel Messi ana miaka 30 na ndiye wa pili kwa thamani, thamani yake ikiwa $242.8m?

Mbona? Moja ya sababu za mchezaji huyo wa Argentina kuwa na thamani ya juu ni kutoshuka kwa kiwango chake, na mwendelezo wa kasi ya ufungaji mabao.

Messi amefunga mabao kumshinda Ronaldo msimu huu (20 na Ronaldo 16), pamoja na kusaidia ufungaji wa mabao mengi (tisa dhidi ya matatu).

Aidha, kinyume na mwenzake wa Ureno, ligini ufungaji wake haukushuka ukilinganisha na msimu uliotangulia.

Ronaldo aliyetikisa wavu mara 25 La Liga 2016/17 msimu huu amefunga mara nne pekee. Messi anakaribia kufunga bao lake la 20.

Jambo jingine linalozingatiwa ukikadiria thamani ni jinsi mchezaji amejifunga kwa klabu ya sasa. Hakuna wachezaji wengi ambao wamekaa klabu moja kama Ronaldi.

Licha ya uvumi mara kwa mara kwamba anaweza kuhamia England au Ufaransa, amesalia Real Madrid.

Sababu ni rahisi – kupanda sasa kwa bei ya wachezaji. Mwaka 2009, uhamisho wake ulikuwa wa juu zaidi duniani alipohamia Real. Kwa sasa, bei yake ni ya sita katika orodha ya wachezaji walionunuliwa ghali zaidi.

“Si kwamba Ronaldo amepoteza thamani katika klabu yake, lakini hali kwamba hajahama kwa miaka 10 ina maana kwamba bei yake kwa viwango vya sasa haijulikani,” anasema Poli.

Hilo linasaidia kueleza ni kwa nini Gonzalo Higuaín anamshinda Ronaldo (19 akiwa na thamani ya $135,7 milioni), kwani alinunuliwa na Juventus kutoka Napoli mwaka 2016 kwa zaidi ya $108.1m.

Ni Mei tu ambapo Real Madrid walishinda La Liga na Kombe la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa pamoja, na kuwa klabu ya kwanza kutetea ubingwa Ulaya katika robo karne.

Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya kwa sasa, Real walifika hatua ya muondoano kwa urahisi, licha ya kupitwa na Tottenham Hotspur kwenye kundi – na walishinda mechi nyingi Ulaya hatua ya makundi msimu uliopita.

Real Madrid hata hivyo msimu huu wametatizika La Liga.

Baada ya mechi 18 wamo nafasi ya 4, alama 16 nyuma ya viongozi Barcelona.

“Uchezaji wa klabu pia huchangia thamani ya mchezaji. Msimu huu Real Madrid wamekuwa wanapata kwa wastani chini ya alama mbili kwa mechi La Liga (1.77) ukilinganisha na 2.05 hatua sawa msimu uliopita,” anasema mtafiti huyo.

Lakini, hata hivyo, hilo halina maana kwamba klabu zinaweza kutarajia kumnunua Ronaldo kwa bei ya kutupa.

Kiungo wa Manchester City Kevin de Bruyne, 26, fowadi wa Manchester United Romelu Lukaku na kiungo wa kati Paul Pogba, wote wa miaka 24, ndio wachezaji wengine wanaocheza England walio kwenye 10 bora.

Mshambuliaji wa Real Madrid Cristiano Ronaldo, 32, aliyetawazwa mchezaji bora zaidi wa kiume duniani na Fifa 2017 yumo nafasi ya 49 kwenye orodha hiyo.

Mchezaji mpya wa Barcelona Philippe Coutinho, 25, amewekwa nafasi ya 16 ,thamani yake ikikadiriwa kuwa £33m chini ya bei ambayo Barca walilipa Liverpool kumchukua.

Singida Utd yaigeukia Simba SC
Serikali yatoa agizo zito shule binafsi, mwisho 20/1/2018.