Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameweka wazi sababu za kufanya mabadiliko mara kadhaa kwenye Wizara inayoshughulikia madini nchini.

Akizungumza jana Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuapishwa kwa Mawaziri wapya na Makatibu wakuu wapya, Rais Magufuli alieleza kutoridhishwa na utendaji wa mawaziri katika kusimamia sekta hiyo.

Alisema ingawa Serikali imeshachukua hatua kadhaa za kusaidia kusimamia rasilimali ya madini ikiwa ni pamoja na kufanya marekebisho ya sheria, bado mawaziri husika wameshindwa kufanya kazi ipasavyo hali inayosababisha Tanzania ambayo ni mzalishaji mkuu wa madini Afrika Mashariki kushindwa kuongoza katika mauzo ya madini hayo.

“Hili ni tatizo licha ya kupitishwa kwa sheria ambayo ingesaidia kufanikisha hilo. Ni lazima kuna udhaifu sehemu fulani na mawaziri husika hawawezi kulieupuka hili,” alisema.

Rais Magufuli alieleza kuwa wizara ya madini ilipaswa kufanikisha uwepo wa vituo vya madini katika mikoa kadhaa ambapo madini ya maeneo husika yangekusanywa kabla ya kuuzwa, hali ambayo ingesaidia kuongeza ufanisi katika usimamizi. Alisema hata hivyo wizara ya madini imeshindwa kufanikisha uanzishwaji wa vituo hivyo.

Wiki hii, Rais Magufuli alimuondoa Waziri Angellah Kairuki katika wizara ya madini na kumhamishia katika Wizara ya Uwekezaji ambayo ni wizara mpya. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko alipandishwa kuwa waziri kamili wa wizara hiyo.

Rais John Magufuli akimuapisha Dotto Biteko kuwa Waziri wa Madini

Awali, Profesa Sospeter Muhongo aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini aliondolewa kufuatia mapendekezo ya Tume maalum iliyoundwa kuchunguza usafirishaji wa mchanga wenye madini nje ya nchi, maarufu kama ‘Tume ya Makinikia’.

Wizara hiyo inayoshughulikia madini itakuwa imeongozwa na mawaziri watatu ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Sekta ya madini nchini inakabiliwa na changamoto ya wizi ambapo tangu Rais Magufuli aingie madarakani ameshachukua hatua kadhaa za kipekee kudhibiti wizi huo ikiwa ni pamoja na kujenga ukuta kuzunguka mgodi wa Mererani.

Hata hivyo, bado vitendo hivyo vya wizi havijakoma kwani Januari 4, jeshi la polisi lilifanikiwa kukamata kilo 323.6 za dhahabu zikiwa zinatoroshwa nchini zikisindikizwa na askari nane wasio waaminifu.

Pacquiao aeleza kwanini Mjapan alilia baada ya kupigwa na Mayweather
Video: Zitto Kabwe kuburuzwa mahakamani

Comments

comments