Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amemkana Sylvester Nyegu anayetajwa na upande wa mashtaka kuwa ni msaidizi wake binafsi, katika kesi inayowakabili ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Jana, Agosti 18, 2021 akijibu maswali ya upande wa mashtaka katika kesi hiyo inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Odira Amworo, Sabaya alikana utambulisho wa Nyengu akieleza kuwa hakuwa msaidizi wake.

Sabaya aliieleza Mahakama hiyo kuwa anamtambua Nyegu lakini hakuwahi kuwa msaidizi wake binafsi kama ilivyoelezwa, bali alipangiwa kazi na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai.

Wakili wa Serikali Baraka Mgaya alipomhoji Sabaya kutaka kujua ni kazi gani ambayo Nyegu alipangiwa kwake, Sabaya alijibu kuwa swali hilo aulizwe Nyigu mwenyewe kwakuwa yeye hafahamu alipangiwa kazi kama nani ofisini kwake.

Alipoulizwa kuwa, Agosti 16, 2021 wakati anasomewa mashtaka, Nyegu alikiri kuwa alikuwa msaidizi wake binafsi, Sabaya alisema yeye hakuwa na msaidizi binafsi na kwamba swali hilo aulizwe Nyegu mwenyewe.

Katika hatua nyingine, Sabaya alikataa kuieleza mahakama mambo kadhaa yaliyoulizwa na upande wa mashtaka, akieleza kuwa ilikuwa siri.

Upande wa mashtaka ulitaka kufahamu kuhusu kazi aliyodai kuwa alipangiwa na mamlaka iliyomteua, ambapo awali alieleza kuwa alifika katika duka la Mohamed Saad eneo la bondeni jijini Arusha, kufanya kazi hiyo baada ya kuungana na watu wanne aliowakuta katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.

Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka alimhoji Sabaya, akitaka kujua aliongoza timu hiyo kwenda kufanya kazi aliyodai ni maalum katika duka hilo akiwa kama nani, alisema hawezi kuieleza Mahakama.

Alipoulizwa kuhusu majukumu yake kama Mkuu wa Wilaya ya Hai, Sabaya alisema kuwa hawezi kuyaeleza kwakuwa ni siri.

Wakili Kweka alipomhoji kwa kutumia sheria, akieleza kuwa muundo wa kazi sio siri kwakuwa umewekwa kwenye sheria, bado Sabaya alisisitiza kuwa ni siri.

Wakili: Sabaya utakubaliana na mimi kuwa muundo wa kazi na majukumu sio siri, yameundwa kisheria kwa hiyo sio siri?.

Sabaya: Siri.

Wakili: Kwa hiyo kazi za Kamati zimeanishwa na sheria kwa hiyo sio siri, ni sawa?

Sabaya: Siri.

Wakili: Soma hii Sheria namba 8 ya mwaka 2010 The National Security Council Act, number 2010, section 11.

Sabaya anasoma:

Wakili: Kwa hiyo majukumu ya Kamati ya Ulinzi na usalama yanajulikana na kila mtu akitaka anaweza kuisoma

Sabaya: Ndio zimeainishwa

Kesi hiyo iliahirishwa na itaendelea kusikilizwa leo, Agosti 19, 2021.

Gomes uso kwa macho na Sven Vandebroeck
Aliyekuwa Rais wa Afghanistan alia kuangushiwa jumba bovu