Katika kufanikisha malengo ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Serikali imesema itaendelea kutumia lugha ya Kiswahili kama bidhaa ambayo hivi karibuni imetajwa kuwa moja ya lugha adhimu inayotumiwa na Mataifa mbalimbali Ulimwenguni.

Balozi, Agnes Kayola ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Wanahabari yanayofanyika Bagamoyo Mkoani Pwani, na kuhimiza Vyombo vya Habari kuendelea kuitumia lugha ya Kiswahili kwa Ufasaha.

Balozi Agnes Kayola amefingua mkutano huo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Joseph Sokoine.

Amesema sambamba na hatua hiyo, pia wanakusudia kuibua fursa zilizopo katika Nchi Wanachama wa SADC, kwa kuendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ikiwemo vyombo vya Habari.

Balozi Agnes amesema, “Tunalenga kuwajengea uelewa Wanahabari juu ya kazi za SADC, wao washiriki kuiarifu jamii hasa ya Watanzania kuzitambua fursa zilizopo na hii ni muhimu ikaendana na matumizi ya lugha ya Kiswahili.”

Hata hivyo katika mafunzo hayo Wanahabari wameaswa kuzingatia namna ambavyo wanaweza kuripoti habari za SADC kwa usahihi kwa kuielekeza jamii kazi zinazofanywa katika.kuimarisha uhusiano na kuibua shughuli za kiuchumi.

Katika mafunzo hayo, baadhi ya wanahabari walipata fursa ya kuuliza maswali ambayo mengi kati ya hayo yalijielekeza katika kutaka kufahamu namna SADC inavyoshughulikia matatizo ya baadhi ya nchi zenye mgogoro ikiwemo ule wa nchi ya Jamhuri ya Kidemorasia ya Kongo DRC na Rwanda.

Akijibu maswali hayo, Balozi amesema tayari hatua kadhaa zimechukuliwa kama njia za awali katika kuhakikisha amani ya ukanda huo inapatikana.

Mafunzo hayo ya siku mbili ya Wanahabari ambayo yameratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ), yaliyoanza hii leo Julai 25, 2022, yanatarajia kumalizika kesho Julai 26, 2022.

WHO yataka juhudi kupunguza vifo majini
Madereva watakiwa kujiepusha na migomo