Wakati timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ ikiondoka leo Novemba 8, 2016 kwenda Yaoundé, Cameroon kwa ajili ya mchezo wa kimataifa wa kirafiki, Vijana wa Tanzania maarufu kwa jina la Serengeti Boys, wao wanatarajiwa kuondoka kesho Novemba 9, 2016 kwenda Korea Kusini, kupitia Dubai, Falme za Kiarabu.

Twiga Stars imeondoka na nyota 17 na viongozi sita kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya (KQ) ambapo walipita Nairobi- Kenya ilihali Serengeti Boys kwa upande wao watatumia ndege ye Emirates katika safari itakayoanza saa 10.30 jioni.

Inakwenda kushiriki michuano maalumu ya kimataifa ya vijana ambapo itaripoti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, kuanzia saa 7.00 mchana.

Wakati Serengeti wakiwa wamealikwa huko Korea Kusini, Twiga Stars wao wamealikwa na Waandaaji wa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wanawake 2016 – Cameroon ambao wameamua kuipa heshima Tanzania na kuona kuwa timu hiyo ina ubora wa na kwamba inafaa kupimana ubavu kabla ya kuanza kwa fainali hizo Novemba 19, mwaka huu.

Twiga Stars ambayo sehemu kubwa ya kikosi hicho kinaundwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Wanawake ya Tanzania Bara yaani Kilimanjaro Queens ina rekodi nzuri ya kuwa kinara wa viwango vya ubora kwa nchi za Afrika Mashariki na kati, lakini zaidi ni mabinga wapya wa ukanda huo – ubingwa uliopatikana mwezi Septemba, mwaka huu huko Uganda.

Rekodi hizo zimesukuma Shirikisho la soka nchini Cameroon (FECAFOOT) – nyumbani kwa Rais wa CAF, Issa Hayatou kuikubali Twiga Stars na hivyo kuomba kucheza nayo mwishoni mwa juma hili. Tayari Twiga Stars imefanya maandalizi ya kutosha chini ya Makocha Sebastian Nkoma na Wasaidizi wake Edna Lema na El Uterry Mohrery.

Kikosi cha Twiga Stars kinaundwa na makipa, Fatma Omari na Najiat Abbas; mabeki ni Wema Richard, Sophia Mwasikili, Anastasia Katunzi, Maimuna Hamisi, Fatuma Issa, Happiness Mwaipaja na Mary Masatu wakati viungo ni Donisia Minja, Stumai Abdallah, Amina Ally, Anna Mwaisura na Fadila Kigarawa ilhali washambuliaji ni Fatuma Swalehe, Asha Rashid na Mwanahamisi Omari.

Vijana wanaosafiri kesho ni makipa Ramadhani Kabwili, Kelvin Kayego na Samwel Brazio; mabeki ni Shomari Ally, Israel Mwenda, Nickson Kibabage, Dickson Job, Ally Msengi na Enrick Vitalis wakati viungo ni Ally Ng’anzi, Shaban Ada, Asad Juma, Issa Makamba huku washambuliaji wakiwa ni Muhsin Makame, Ramadhani Gadaffi, Rashid Chombo, Cyprin Mtesigwa na Mohammed Abdallah.

Kwa upande wa Taifa Stars, kikosi cha Kocha Mkuu wa Timu ya soka ya Tanzania, Charles Boniface Mkwasa kinatarajiwa kuondoka Ijumaa Novemba 11, mwaka huu kikiwa na nyota 20 kati ya 24 waliotangazwa wiki iliyopita. Stars inakwenda Harare, Zimbabwe kucheza na wenyeji kwenye mchezo wa kirafiki wa kimataifa utakaofanyika Novemba 13, mwaka huu.

Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki utakaofanyika jijini Harare, umeratibiwa kwa mujibu wa kalenda ya Shirikisho soka duniani (FIFA).

Shirikisho la soka nchini Zimbamwe liliiomba TFF mchezo huo, na kukubalia bila hiyana.

Matokeo ya mchezo huo, ni sehemu malumu kupima viwango vya ubora na uwezo wa timu za taifa. Kwa sasa Tanzania inashika nafasi ya 144 kati ya nchi 205 wanachama wa FIFA zilizopimwa ubora. Zimbambwe yenyewe inashika nafasi ya 110.

Argentina inaongoza ikifuatiwa na Ubelgiji anakocheza Mbwana Samatta – nyota wa kimataifa wa Tanzania. Samatta anacheza klabu ya K.R.C Genk inayoshiriki Ligi Kuu ya Ubelgiji. Timu nyingine bora kimataifa ni Chile, Colombia na Ujerumani.

Katika Bara la Afrika, Ivory Coast ambayo ni ya 31 kwa ubora duniani ndiyo inayoongoza ikifuatiwa na Senegal (32), Algeria (35), Tunisia (38) na Ghana (45).

Antonio Conte Kujaribu Tena Kwa Leonardo Bonucci
Mkataba Wa Hector Bellerin Wanukia Emirates Stadium