Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Burundi Saido Ntibazonkia huenda akaondoka Young Africans kufuatia taarifa za kunyemelewa na viongozi wa timu moja kutoka Uarabuni.

Taarifa hizo zimeeleza kuwa Viongozi wa klabu hiyo ya Uarabuni wamemfuata Saido nyumbani kwao Burundi ili kufanya naye mazungumzo ya kumsajili.

Mtu wa karibu na mchezaji huyo, amesema: “Hivi karibuni Saido akiwa kwao Burundi alifanya kikao na mwakilishi wa timu kutoka Uarabuni ambayo siwezi kuitaja.”

“Anaweza kukubali dili hilo maana lina pesa nyingi, ila kwa upande wa viongozi wa Young Africans wamemwambia asubiri wakimaliza Mapinduzi wataongea naye kujadili mkataba mpya.”

Saido alisajiliwa Young Africans wakati wa dirisha dogo la msimu uliopita, na mwishoni mwa msimu huu mkataba wake na klabu hiyo utafikia kikomo.

Saido aliondoka nchini kuelekea nyumbani kwao Burundi mara baada ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC, kwa ajili ya mapumziko ya muda mfupi, na tayari amesharejea nchini (Zanzibar) kwa ajili ya mchezo wa Nusu Fainali ya Michuano ya Mapinduzi inayoendelea visiwani Zanzibar.

Kaze: Hakuna Staa Young Africans
Country Boy ajitoa Konde Gang