“Wagosi wa Kaya”, Coastal Union ya Tanga umelitupia lawama za moja kwa moja Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) pamoja na Bodi ya Ligi (TPLB) kwa kuchangia timu yao kushuka daraja.
Coastal ambayo iliwahi kutwaa taji la Ligi Kuu Bara (wakati huo Ligi Daraja la Kwanza) mwaka 1988, imeshuka daraja wikiendi iliyopita baada ya kufungwa mabao 2-1 na Stand United.
Kwa sasa timu hiyo inaburuza mkia kwa kuwa na pointi 22, ikiwa na mchezo mmoja kukamilisha msimu ambao hata kama ikishinda hauwezi kuwasaidia kutoshuka daraja.
Kaimu Katibu Mkuu wa Coastal Union, Salim Bawazir, amesema upangwaji mbovu wa ratiba ya ligi msimu huu ndiyo umechangia wao kushuka daraja msimu huu.
“Waliopanga ratiba ndiyo waliochangia kwa kiasi kikubwa sisi kushuka daraja, angalia tumeenda Shinyanga mara tatu kucheza dhidi ya Mwadui, Stand na Kagera Sugar wakati timu zingine zikienda mkoa wenye timu tatu au mbili, basi zinacheza mechi zote kwa safari hiyo moja.
“Angalia kwa sasa tumebakiwa na mchezo mmoja tu wakati nyingine zina michezo miwili mpaka mitatu, kiukweli hatukutendewa haki, wachezaji wetu walikuwa wakipambana kuipigania timu yao lakini masuala kama haya ndiyo yametufelisha,” alisema Bawazir.
Bawazir alisema wanasubiri ligi iishe ili wafanye kikao na mshauri mkuu wao, Nassor Binslum na Chama cha Soka Mkoa wa Tanga kupanga mikakati ya kurejea Ligi Kuu Bara msimu wa 2017/2018.
Chanzo: CHAMPIONI

Wamuuzi Wa Taifa Stars Vs The Pharaohs Wafahamika
Arsene Wenger Amtengea Kiungo Wa Uswiz Mamilion Ya Pauni