Wasafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam wamelalamikia upandishwaji wa gharama za ukaguzi maalum wa makontena (scanning) zinazochajiwa na Kampuni ya TICTS.

Wasafirishaji hao wa mizigo wameeleza kuwa kwa sasa TICTS wameanza kutoza kiasi cha shilingi 340,000 kwa kontena lenye urefu wa futi 40 na shilingi 225,000 kwa kontena lenye urefu wa futi 20, madai ambayo TICTS wameyakanusha wakieleza kuwa bei hizo ziko kisheria.

Sakata hilo limeibuka ikiwa ni miezi michache imepita baada ya Rais John Magufuli kuagiza kila kontena linalopita bandarini hapo kufanyiwa ukaguzi kwa mashine maalum (scanning).

Aidha wasafirishaji hao wameeleza kuwa ingawa Rais Magufuli aliagiza kila kontena kukaguliwa kwa njia hiyo, hakuagiza kupandishwa kwa gharama za ukaguzi huo, hali wanayodai imetumiwa vibaya na TICTS.

Wameonya kuwa ongezeko hilo la gharama linaweza kuigharimu Bandari ya Dar es Salaam kwa kupandisha gharama, hivyo kupelekea baadhi ya wafanyabiashara kukimbilia katika Bandari nyingine za nchi jirani.

Mjumbe wa Bodi ya Umoja wa wamiliki magari ya mizigo (Tatoa), Rahim Dossa alieleza kushangazwa na ongezeko hilo la bei huku akidai kushangazwa zaidi na kitendo cha mizigo ya Rwanda kutochajiwa bei hiyo.

“Wasafirishaji wa mizigo kwenda Rwanda hawahusiki na ongezeko hili la bei la Ticts, kwahiyo wa Rwanda hawalipi gharama za kufanyiwa ukaguzi huo. Tunashangaa kwanini kunakuwa na ubaguaji huu,” Dossa anakaririwa na The Citizen.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA), Deusdedit Kakoko alisema kuwa mgogoro huo kati ya Ticts na Tatoa uko mikononi mwa Sumatra.

“Sisi hatuhusiki na mgogoro wa aina hiyo. Tuko hapa kuchapa kazi na siko tayari kutoa maelezo zaidi kwa sababu msingi wa kazi ya TPA ni tofauti kabisa na Ticts,” alisema Kakoko.

Mbowe avunja Ukimya kupotea kwa Saanane, atahadharisha ‘maneno’
Mzee Kingunge aeleza kwanini Wapinzani hawatashinda 2020 kwa hali hii