Kamanda wa Polisi Mkoani Mwanza, Jonathan Shanna ametolea ufafanuzi suala la kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi wa Fedha na Mipango wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa  Bugando BMC, Mtawa Suzan Bartholomew mara baada ya taarifa nyingine kusambaa zikieleza kuwa huenda aliuawa kwa kusukumwa na mtu au watu wasiojulikana.

Hapo awali taarifa ilikuwa ni kwamba Mtawa huyo alijiua kwa kujirusha ghorofani na kupelekea kuumia vibaya mpaka kulazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU)  na kuendelea kupatiwa matibabu, alifariki dunia usiku wa Agosti 28.

Shanna, amesema kuwa taarifa juu ya mtawa huyo kuuliwa sio za kweli kwa kuwa vipo vielelezo vingi vinavyoonesha kuwa mtawa huyo alijiua mwenyewe, ikiwamo ushahidi wa maandalizi ya kujiua ikiwa pamoja na picha ya kamera (CCTV) iliyomuonesha akiwa anapanda ngazi kwenda eneo alilojirusha.

“Kwenye uchunguzi kuna mambo mengi, picha ya kamera ya CCTV  ipo wazi, inamuonesha mtawa huyo akiwa anapanda ngazi kwenda eneo husika na alipojirusha kuna baadhi ya wafanyakazi wengine na wagonjwa ambao walimuona hivyo hakuna taarifa za kusukumwa wala kurushwa.

Kamanda Shanna pia amesema amesema kabla ya kujirusha, Mtawa huyo  alifungasha vitu vyake  katika nyumba aliyokuwa akikaa ikiwa ni pamoja na kumkabidhi mmoja wa ndugu zake gari lake na picha zake na baba yake mzazi akimueleza kuwa anakwenda eneo asilolijua.

“Kabla ya tukio hilo Mtawa huyo alijiandaa na kufunga vitu vyake, aligawa baadhi ya vitu kwa watu ikiwa ni pamoja na kumpatia gari mmoja wa ndugu zake na picha zake na wazazi wake, aliziondoa line za simu zake kutoka ndani ya simu na kuweka simu juu ya kiyoyozi eneo ambalo alijirusha,” alifafanua.

Kamanda Shanna alisema yeye binafsi alitembelea eneo alikojirusha Mtawa huyo na kupata maelezo kwa watu mbalimbali.

 

 

Kiba ajiunga na kambi ya Coastal Union
Sababu watumiaji 110 kuacha kutumia ARV Muhimbili zatajwa