Wadhamini wakuu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania wanafuatilia kwa ukaribu na umakini sana sakata la upangaji matokeo kwa timu nne za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambazo zimeshushwa daraja na tuhuma za viongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na klabu kujihusisha na suala hilo.

Ufuatiliaji huu wa Vodacom umeanza siku moja baada ya kuwepo taarifa kuwa Kampuni ya Geita Gold Minning imevunja mkataba wa kuidhamini timu ya Geita Sports wenye thamani ya Tsh. milioni 300 kutokana na kukutwa na hatia kuhusishwa na upangaji matokeo katika mchezo wake wa mwisho dhidi ya JKT Kanembwa ambapo Geita ilishinda bao 8-0.

Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina Nkurlu amesema kuwa, wameamua kulifuatilia kwa makini suala hili kwa kuwa ligi hiyo ndiyo inatoa timu tatu bora zinazopanda daraja na kushiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara ambao wanaidhamini.

“Tunadhamini Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara kwa lengo la kukuza mchezo wa soka nchini, tunapenda kuona malengo yetu ya kukuza soka hapa nchini yakirandana na  kufuatwa kwa sheria zote za ili tuendeleze mchezo huu nchini na ngazi ya kimataifa na kuboresha maisha ya wachezaji pia mchezo kuchangia pato la serikali kupitia kodi.”

“Napenda kuwasihi viongozi wa soka kuzingatia sheria kwa umakini ili malengo haya yaliyokusudiwa yaweze kufikiwa”, alisema Nkurlu.

Matina Nkurlu-Meneja Uhusiano wa Vodacom TanzaniaMeneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania – Matina Nkurlu

Timu nyingine zilizoshushwa daraja katika uamuzi wa  Kamati ya Nidhamu ya TFF ambayo ilibainisha kuwa baadhi ya viongozi wa soka wameshiriki kwenye sakata hilo  ni Polisi Tabora na JKT Oljoro ambapo kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo, Polisi ilishinda kwa mabao 7-0.”

Uamuzi huo ulitolewa baada ya kamati hiyo kukaa vikao vitatu na kuwahoji viongozi wa timu, wachezaji, makocha pamoja na waamuzi na makamisaa wa mechi hizo.

Polisi Tabora na JKT Oljoro  zimeshushwa mpaka Ligi Daraja la Pili (SDL) sanjari na Geita huku JKT Kanembwa ikishushwa hadi ligi ya mkoa.

Waliofungiwa kuhusika na masuala ya soka maisha yao yote ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora, Yusuph Kitumbo, Mwenyekiti wa JKT Oljoro Amos Mwita, Kocha Msaidizi wa Tabora, Katibu wa chama cha mchezo huo Tabora, Fateh Remtullah, kocha msaidizi wa Geita, Choki Abeid na Katibu wa Polisi Tabora, Alex Kataya, mwamuzi na kamisaa wa mchezo wa JKT Kanembwa na Geita Gold Sport.

Waliofungiwa kujihusisha na soka kwa miaka 10 na faini ya Sh 10 milioni ni mlinda mlango wa Geita Denis Richard ambaye alikuwa anacheza kwa mkopo timu hiyo akitokea timu ya vijana ya  Simba na waamuzi Hamis Mchunde na Masoud Mkelemi, kipa wa JKT Kanembwa, Mohamed Mohamed aliyekiri kupokea sh 300,000.

Kocha Wa Twiga Stars Abebeshwa Jukumu Zito Zanzibar
Young Africans Waendelea Kulia Na Ratiba Ya Kombe La Shirikisho