Kesi zilizofunguliwa mahakamani dhidi ya Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) Ravia Idarous na viongozi wenzake, huenda zikamuengua katika orodha ya wagombea urais wa chama hicho.

Uchaguzi mkuu wa ZFA unatarajiwa kufanyika kisiwani Pemba Aprili 14, ambapo Ravia ameomba kutetea nafasi yake, akikabiliwa na upinzani kutoka kwa kocha wa zamani wa Zanzibar Heroes Salum Bausi.

Jana, Bausi aliwasilisha katika kamati ya uchaguzi barua inayoonesha sababu lukuki kutaka mpinzani wake ang’olewe kwa kuwa amepoteza sifa.

Katika barua hiyo ya Aprili 6, 2016, Bausi ameanika sababu kuu tatu kuitaka kamati imuondoe Ravia katika resi za kugombea kiti cha urais wa chama hicho.

Bausi alieleza kuwa, katika kipindi cha uongozi wa Ravia akiwa Rais wa ZFA, amekiendesha kwa misingi ya kisiasa kupitia vikao halali, kinyume na kifungu cha 4 cha katiba ya ZFA.

“Kupitia vikao hivyo, akiwa Rais amewahi kusema kwamba mpira hauwei kuchezwa hapa Zanzibar hadi Muungano uvunjike au kuwe na serikali tatu,” Bausi alinukuu maneno ya Ravia katika moja ya vikao vya ZFA.

Aidha amedai kuwa, akiwa Rais, Ravia amesababisha ZFA kutokuwa na uhusiano mzuri wa kimichezo na nchi nyengine hivyo kuiweka katika tishio la kuweza kufutiwa uanachama wa CAF na CECAFA.

Ametaja vifungu namba 7 (h), (k) na (o) vya kanuni za usajili wa vyama vya michezo 2004, na kanuni namba 19 kifungu (d) (iii) cha sheria ya Baraza la Michezo la Taifa Zanzibar (BTMZ) namba 10/2010, kuwa vinathibitisha ukiukwaji huo.

Aidha amefahamisha kuwa, barua ya Kamishna wa Polisi yenye namba ya kumbukumbu PHQ/Z/C.5/4/4MJN/VOL. XII/134 ya Novemba 24, 2015 inaunga mkono pingamizi alizomuwekea mgombea huyo.

Madai mengine aliyoonesha kwenye barua yake hiyo, ni kuwepo shutuma za ubadhirifu wa hali ya juu wa fedha za ZFA unaomuhusisha Ravia na wenzake.

Bausi ameeleza kuwa, kutokana na shutuma hizo nzito pamoja na kuwepo kesi ya jinai juu yake, kunamuondolea Ravia sifa ya uadilifu unaomfanya asifae kuwa kiongozi wa ZFA.

Alifahamisha kuwa, barua ya Kamishna wa Polisi Zanzibar yenye namba ya kesi CID/HQ/IR.1/2015 ya Disemba 23, 2015 na ile ya Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai namba CID/HQ/Z/C.5/18/61 ya Novemba 2014 zinazoonesha kuwepo kesi za jinai dhidi ya Ravia, ni kielelezo tosha cha kutokumpitisha kugombea.

Bausi alisema, katika uongozi wa Ravia, kulikuwa na utawala mbaya katika uendeshaji soka sambamba na kupindwa kwa katiba na kanuni hali iliyoibua kesi kadhaa mahakamani, ikiwemo namba 62/2014.

Aidha, alisema kuna kesi nyengine ambazo bado ziko mahakamani hadi sasa, ambazo zote zimeibuka katika kipindi cha uongozi wa mlalamikiwa.

Katika pingamizi hiyo, Bausi pia ameambatanisha vielelezo vyote ikiwemo barua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa ZFA iliyoandikwa Oktoba 29, 2015 kukazia madai yake.

Kwa hivyo, ameitaka kamati ya uchaguzi, kufanya haki kwa kumfuta mgombea huyo hadi atakaposafishwa na mahakama kutokana na rundo la kesi zinazomkabili.

Romelu Menama Lukaku Kuuzwa Kwa Masharti
Thiago Silva Asikitishwa Na Maamuzi Ya Man City