Kocha wa klabu ya DC United inayoshiriki ligi kuu ya soka Marekani (MLS) Ben Olsen amethibitisha kuwa katika mpango wa kumsajili mshambuliaji kutoka England na klabu ya Everton Wayne Mark Rooney.

Olsen amethibitisha mchakato huo alipohojiwa na tovuti ya TMZ, ambapo alisema dhamira yake kubwa ni kutaka kukamilisha uhamisho wa mshambuliaji huyo, ambaye aliwahi kuwa nahodha wa timu ya taifa ya England.

Kocha huyo alisema Rooney ni mshambuliaji ambaye anaamini atakisaidia kikosi chake katika harakati za kufanya vyema msimu huu katika ligi ya Marekani, na atapambana kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.

“Lengo langu ni kutaka kufanya kazi na Rooney, naamini hata yeye anahitaji kucheza soka hapa Marekani, kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa mshambuliaji huyu atatua DC United.” Alisema Olsen

Wakati kocha huyo wa DC United akionyesha kuwa na matumaini ya kufanya kazi ya Wayne Rooney, meneja wa klabu ya Everton Sam Allardyce, amepinga mchakato huo kwa kusema mpaka jana Ijumaa mchezaji huyo alikua hajawasilisha ombi lolote la kutaka kuondoka.

Allardyce amesema kuna haja ya mpango wa Rooney ukafuatwa na sio kuzipa nafasi taarifa zinaotoka Marekani, ambazo amedai zinawachanganya mashabiki wa klabu hiyo ya Goodison Park.

“Kama mchezaji anataka kuondoka, sitomzuia, lakini utaratibu si unatakiwa kufuatwa ili mambo yaende katika utaratibu unaotambulika, sio mtu anaibuka katika vyombo vya habari na kueleza anataka kumsajili,” Amesema Allardyce katika mkutano na waandishi wa habari.

“Kwa uelewa wangu jambo hilo lina dalili zote za kufanikiwa, lakini ninasisitiza utaratibu, ili tujenge heshima ya pande zote mbili ambazo zitakutana kuzungumzia suala la kuondoka kwa Rooney.

“Sina nia mbaya wala sitaki kueleweka kama nina dhamira ya kutaka kukwamisha mchakato wa kuondoka kwa mshambuliaji huyu, nitafurahi akiondoka kwa sababu atabadilisha mazingira ya soka lake.”

Rooney mwenye umri wa miaka 32, ameshaonesha nia ya kutaka kuihama Everton ambayo ilimsajili mwezi Julai mwaka 2017 akitokea Man Utd, na tayari ameshaifungia The Toffees mabao 11.

Hii ni mara ya pili kwa Rooney kuitumikia Everton, kwani alikuwepo klabuni hapo tangu akiwa na umri mdogo na alianza kucheza katika kikosi cha kwanza akiwa na umri wa miaka 18 mwaka 2004, na baadae alisajiliwa na Man Utd.

Mkataba wake na klabu ya Everton utafikia kikomo mwaka 2020, na kama kuna klabu yoyote itahitaji kumsajili katika kipindi hiki haina budi kukaa chini ili kujadilina kwa kina na uongozi wa The Toffees.

Ummy awatoa hofu watanzania juu ya Ebola
Neymar: Ninahitaji sana kuichezea timu yangu