Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ameahidi wafanyakazi wote kuwepo kwa nyongeza ya mishahara kufikia sherehe za siku ya wafanyakazi (Mei Mosi), 2022 ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 1 mwezi Mei.

Rais Samia ametoa ahadi hiyo leo Mei 1, 2021 wakati akijibu malalamiko ya wafanyakazi kutokupandishwa mishahara kwa muda mrefu, katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitaifa yaliyofanyika uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.

Aidha, ameeleza matamanio yake kwa wafanyakazi huku vakiweka bayana kuwa ameshindwa kutimiza hilo kwa mwaka huu kutokana na kushuka kwa uchumi wa nchi kutoka asilimimia 6.9 hadi asilimia 4.7 kulikosababishwa na janga la Corona.

“Mishahara haijaongezwa kwa muda mrefu, mimi binafsi natamani kuongeza mishahara mwaka huu ila kwa sababu mbalimbali nimeshindwa, uchumi wa Tanzania umeshuka kutoka 6.9% hadi 4.7% kwa sababu ya Corona, mwakani siku kama ya leo nitapandisha mishahara,” amesema Rais Samia.

Kuhusu madeni ya Watumishi Serikali, Rais Samia amesema Serikali inajitahidi kulipa na katika kipindi cha Julai mwaka jana hadi Aprili mwaka huu Serikali imelipa malimbikizo ya mishahara yenye thamani ya Sh. Bil. 74 kwa Watumishi 36,126 na itaendelea kulipa madeni yote ya Watumishi.

Akizungumzia ucheleweshwaji wa malipo kwa wastaafu Samia ameeleza kusikitishwa na jambo hilo huku akieleza kuwa wataanza kulipwa kuanzia mwezi huu ( Mei) na zoezi hilo kuendelea mpaka watakapoisha.

“Kuhusu ucheleweshwaji wa malipo kwa Wastaafu hili lipo na linanisikitisha sana, natamani kuona Mtu akistaafu analipwa mara moja badala ya kuzungushwa, wale Wafanyakazi ambao wamerundikana tutaanza kuwalipa mafao yao kuanzia mwezi huu na kila mwezi,” amesema Rais Samia

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 3, 2021
JKT: Warudi kambini