Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu wenye mashaka iwapo ataweza kuimudu nafasi hiyo.

Akizungumza katika Viwanja vya Jamhuri jijini Dodoma katika hafla ya kuuaga mwili wa Hayati Dkt John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Tanzania, Samia amewaahidi Wananchi kuwa hakuna kitakachoharibika.

“Kwa wale ambao wana mashaka kwamba Mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye maumbile yake ni Mwanamke” amesema Rais Mama Samia.

Samia ametumia nafasi hiyo kumuelezea Hayati Dkt John Pombe Magufuli kama Kiongozi aliyekuwa mcha Mungu, mnyenyekevu, mchapakazi, msikivu na mcheshi.

Mbali na hilo, Rais Samia ameeleza kuwa kwa mara ya mwisho alizungumza na Hayati Dkt Magufuli wakati akielekea katika ziara mkoani Tanga, huku akimtaka kutokuwa na wasiwasi na kwenda kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi pamoja na kuwafikishia Wananchi salamu zake za upendo, “sikujua kama maneno yale yalikuwa ya kuniaga na kuwaaga Watanzania,” amesema Rais Samia.

Samia pia amesmshukuru Hayati Dkt Magufuli kwa imani, heshima na nafasi alivyompa enzi za uhai wake ambavyo vimemfanya awe Makamu wa Kwanza wa Rais Mwanamke na sasa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Machi 23, 2021
Trump asivyokubali kushindwa