Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa semina ya chama cha wabunge wanawake wa mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai ameyasema hayo Jijini Dodoma na kuongeza kuwa chama hicho kimeandaa semina yenye lengo la kuwahamasisha wajumbe wake mambo mbalimbali hasa ushiriki katika chaguzi mbalimbali.

“Chama cha wabunge wanawake wa mabunge ya Jumuiya ya Madola Kanda ya Afrika kimeandaa semina ya kuwahamasisha wajumbe wake kuhusu maswala mbalimbali yanayowahusu na itafanyika Oktoba 26 hadi 29, 2019 Jijini Arusha,” amesema Ndugai

Spika Ndugai ameongeza kuwa kutakuwepo na washiriki takribani 50 kutoka nchi 18 za Jumuiya ya Madola zikiwemo Afrika Kusini, Botswana, Cameroon, Eswatini na nchi nyingine ambazo zitaainishwa.

Amebainisha kuwa miongoni mwa wageni watakaohudhuria ni Spika wa Bunge la Afrika Mashariki na Mabalozi wa nchi 17 za Afrika ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya madola, Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Balozi wa Pakstani, Mawaziri na viongozi wanawake, viongozi wa dini na wawakilishi kutoka UN.

Ndugai amefafanua kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndio makao makuu ya chama cha Mabunge ya Jumuiya ya Madola kanda ya Afrika ambayo ina wabunge wanachama kutoka nchi 18 za Jumuiya  ya Madola zilizopo katika bara la Afrika na mabunge mengine 46 ya majimbo kutoka Afrika kusini 9, Nigeria 36 na Tanzania moja.

Semina hiyo itakayo beba kauli mbiu ya “Kuboresha ushiriki wa wanawake katika michakato ya uchaguzi” pamoja na Mambo mengine itajadili kuboresha ushiriki wa wanawake katika michakato ya uchaguzi.

TRA: Atakayefichua Wakwepa Kodi atalipwa 3% ya Kodi Itakayokombolewa
Video: Harmonize amtaja Chibu na Zari kwenye ngoma yake mpya 'Uno' sikiliza hapa