Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia mwaka 2015 Samia Suluhu Hassan, ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leo Machi 19, 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma katika Ikulu ndogo jijini Dar es Salaam.

Samia ameapishwa kuwa Rais kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, 2021 katika Hospitali ya Mzena, mkoani Dar es Salaam.

Samia Suluhu Hassan, Rais wa sita wa Tanzania anakuwa mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania kushika wadhfa huo lakini pia ni ni mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya Makamu wa Rais.

Viongozi mbalimbali wameshuhudia hafla hiyo akiwemo Rais mstaafu wa awamu ya Nne, Jakaya kikwete na Rais wa Pili wa Tanzania Ali Hassan Mwinyi.

Julai 2015 Hayati Dkt. John Magufuli alimteua Samia Suluhu Hassan  kuwa mgombea mwenza wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika  uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Baadaye alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza Mwanamke katika historia ya nchi baada ya ushindi wa Dkt Magufuli katika uchaguzi huo wa mwaka 2015.

Kutokana na utumishi wake mahiri, Dkt John Magufuli alimteua kwa mara nyingine Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea Mwenza wa nafasi ya Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika mwezi Oktoba mwaka 2020.

Simba, Young Africans zampongeza Rais Samia
Samia kuapishwa kuwa Rais wa Tanzania leo