Aliyekua kiungo wa klabu bingwa nchini England Manchester City Samir Nasri ameongezewa adhabu ya kufungiwa kucheza soka, kufuatia kosa la kutumia dawa za kusisimua misuli.

Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limetangaza kumuongezea adhabu kiungo huyo kutoka nchini Ufaransa, kwa kumfungia kwa kipindi cha miezi 18 sawa na mwaka mmoja na nusu.

Awali kiungo huyo alikua amedhibiwa kutumikia adhabu kwa kipindi cha miezi sita, lakini alichukua hatua ya kukata rufaa iliyopinga maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yake.

Maamuzi ya kupinga adhabu iliyotolewa awali na shirikisho la soka barani Ulaya UEFA na kulazimika kufufuliwa upya kwa kesi yake, yamekua chagizo la kuongezewa adhabu hiyo, baada ya uthibitisho kuonyesha kwa mara ya pili alitumia dawa hizo akiwa na klabu ya Sevilla CF aliyomsajili kwa mkopo akitokea Man City mwaka 2017.

“Mchezaji Samir Nasri ameadhibiwa kwa muda wa miezi 18, na adhabu hii inaanza kufanya kazi kuanzia Julai mosi 2017,”  imeeleza taarifa iliyochapishwa kwenye Tovuti ya UEFA.

“Samir Nasri ataruhusiwa kurejea katika mazoezi na kucheza soka la ushindani kuanzia Novemba mosi 2018.”

Uhakika wa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 kutumia dawa hizo ulithibitishwa na taasisi ya kupinga dawa za kusisimua misuli duniani WADA (World Anti-Doping Agency), lakini kwa mara ya pili UEFA walijiridhisha kupitia taasisi ya kupinga dawa za kusisimua misuli ya Ufaransa (French Anti-Doping Agency) pamoja na mkaguzi maalum kutoka kamati ya nidhamu ya shirikisho hilo.

Vipimo vya awali vilivyofanywa na WADA kwa mara ya kwanza, ndivyo vilivyotumiwa na kwa mara ya pili na French Anti-Doping Agency pamoja na mkaguzi maalum kutoka kamati ya nidhamu ya UEFA, na bado majibu yalionyesha Nasri alitumia dawa hizo.

Kwa sasa Samir Nasri anaitumikia klabu ya Antalyaspor ya Uturuki na msimu wa  2017/18 alicheza michezo minane na kufunga mabao mawili.

Benki M yafilisika, yachukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania
Kwandikwa aipa tano Tanrods Manyara