Joto lililokuwa linapasha kiti cha Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho jana lilitulizwa na ubaridi mwororo wa goli la ushindi dhidi ya Newcastle lililofungwa na Alexis Sanchez.

Ni kama Sanchez alikilinda rasmi kibarua cha Mourinho kwa goli lake la tatu katika kipindi cha pili, lililosababisha Wekundu hao wa Old Trafford kujipatia ushindi wa 3-2, ingawa katika kipindi cha kwanza chote walikuwa wameelemewa na mzigo wa magoli mawili-patupu.

Ushindi huo ulifuta ugonjwa wa kukosa ushindi  kwa takribani mechi nne, kipindi kilichomnyong’onyeza Mourinho na mashabiki wa klabu hiyo.

Magoli ya Newcastle yalipachikwa na Kenedy pamoja na Yoshinori Muto, lakini katika kipindi cha pili Manchester walirudi na nguvu ya aina yake, Juan Mata na Anthony Martial wakaweka usawia wa magoli kabla Sanchez hajapeleka kilio rasmi Newcastle.

Baada ya ushindi huo, Mourinho alirusha makombora kwa vyombo vya habari akidai kuwa vimekuwa vikimuwinda na kumvalisha makosa ambayo sio yake, akitolea mfano wa mambo ambayo anaweza kupakaziwa kuwa chanzo ambayo yako nje ya uwezo wake.

“Nitaenda London usiku huu, lakini kama mvua itanyesha kesho huko London, watasema ni kosa langu. Kama kutakuwa na tatizo la Brexit, watasema mimi ndio tatizo,” alisema.

“Sio rahisi kwa wachezaji. Na sio rahisi kwangu pia lakini nadhani maisha yametengenezwa kwa kupata ujuzi wa yanayokutokea, mengine ni mapya na mengine ni yaleyale yaliyowahi kukutokea. Haya ni mapya, hayanifanyi kuwa meneja bora lakini hata kuwa mtu bora,” aliongeza.

“Kuna madhaifu mengi katika kitu ambacho kilipaswa kuwa kizuri. Ninaendana nacho na masikitiko kiasi. Mimi ni mtu mzima, ni mwanaume mkubwa na nitashughulika nacho,” aliongeza.

Kocha huyo maarufu kwa kusema mengi, alikazia kuwa amebaini vyombo vya habari vinamuwinda kwa mabaya lakini ataenda navyo sawa.

Video: Khabib ampiga McGregor, vurugu kubwa zaibuka ulingoni
Bunge lampa ushindi Trump, kelele zatawala

Comments

comments