Kiungo Jadon Sancho amewapa matumaini mashabiki wa Manchester United huenda akajiunga na klabu hiyo wakati wa usajili wa majira ya kiangazi, akitokea Borussia Dortmund.

Sancho ametoa matumaini yayo kwa mashabiki wa Manchester United, baada ya kubonyeza kitufe cha ‘like’ kwenye posti ya Twitter iliyoandikwa “Akili Yake Tayari Ipo Manchester United.”

Kiungo huyo kutoka England aliwekwa benchi katika mchezo uliopita wa ligi ya Ujerumani, wakati klabu yake ya Borussia Dortmund ilipoibanjua RB Leipzig mabao mawili kwa sifuri.

Jambo hilo liliibua minong’ono kwamba winga huyo mwenye umri wa miaka 20, ameshawekwa kando kwenye kikosi hicho kutokana na akili yake kufikiria kuondoka.

Mtangazaji wa mashindano ya Formula 1 huko Ujerumani, Heiko Wasser aliandika Twitter ya kuhusu Sancho kuwekwa benchi, alipoposti: “Akili yake tayari ipo Manchester United.”

Mashabiki wa Man United walichukua posti hiyo na kushea kwenye mitandao ya kijamii, jambo lililokuja kuwafurahisha zaidi baada ya Sancho mwenyewe kuweka ‘like’ kwenye posti inayodai kwamba akili yake ipo Old Trafford.

Shabiki mmoja aliandika: “Akili yake tayari ipo Manchester United. Nasubiri kwa hamu kumwona kwenye kikosi cha United.”

Mwingine aliandika: “Akili ya Jadon Sancho tayari imeshahamia Manchester United.”

Hata hivyo, mkurugenzi wa michezo wa klabu ya Dortmund, Michael Zorc amesema Sancho aliwekwa benchi kwenye mechi ya Leipzig kwa sababu ya uchovu na si kufikiria kuachana na klabu hiyo.

Video: Waziri Mwakyembe "SADC inatambua mchango wa wanahabari katika janga la covid 19"
Gazeti la Tanzania Daima lafungiwa