Mashabiki wa klabu ya Young Africans wanaamini usajili wa Mshambuliaji kutoka Ghana Michael Sarpong, huenda ukawa jibu sahihi la maswali waliokua wanajiuliza, nani atakua mbadala wa David Molinga aliyeondoka klabuni hapo siku kadhaa zilizopita.

Molinga alikua sehemu ya wachezaji walioachwa na uongozi wa Young Africans, kufuatia viwango vyao kutoridhisha msimu uliopita, hatua ambayo ilifungua milango kwa wachezaji wengine kusajiliwa katika kipindi hiki cha kuelekea msimu wa 2020/21.

Sarpong ambaye amejiunga na Young Africans, baada ya kuachwa huru na Rayon Sports ya Rwanda, anakuwa mchezaji wa tatu wa kimataifa kusajiliwa na klabu hiyo msimu huu, baada ya viungo wawili raia wa DR Congo, Tusila Kisinda na Mukoko Tunombe waliotua wakitokea AS Vita ya kwao.

Mwishoni mwa juma lililopita mshambuliaji huyo alikamilisha dili la kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu ya Young Africans, na anatarajiwa kuwa jibu sahihi la mashabiki wa klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika mashariki na kati.

Baada ya kukamilisha dili hilo, Sarpong alisema lengo lake ni kuhakikisha anaisaidia klabu hiyo kufikia malengo yake.

“Ninahisi furaha kuwa mwanafamilia wa Yanga ninatambua hii ni timu kubwa na ina wachezaji wengi wazuri, hivyo nitashirikiana nao kutimiza malengo,” alisema. 

Sarpong mwenye umri wa miaka 24, tayari ameungana na wenzake katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea viwanja vya Chuo cha Sheria jijini Dar es Salaam.

Mashabiki wa Young Africans watakuwa na nafasi ya kuanza kuona ubora wa Sarpong wakati akitambulishwa Agosti 30, mwaka huu, kwenye kilele cha Wiki ya Wananchi, Uwanja wa Mkapa.

Baada ya hapo wanaweza kuushuhudia zaidi ubora wake kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara watakapoanza dhidi ya Tanzania Prisons Septemba 6, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Wabunifu kufaidika na millioni 874
Wajawazito kuendelea na masomo Zimbabwe