Kocha wa Chelsea, Maurizio Sarri ameeleza kusikitishwa na kitendo cha golikipa wa timu hiyo, Kepa Arrizabalaga kukaidi uamuzi wake wa kumtoa nje dakika chache kabla ya mikwaju ya penati dhidi ya Manchester City.

Golikipa wa ziada ambaye kwa maoni ya Sarri alikuwa na uwezo zaidi wa kuzuia mikwaju ya panati, Willy Caballero alilazimika kubaki nje ya chaki akipasha misuli, asiamini kuwa licha ya kibao kuonesha mabadiliko ya yeye kuchukua namba ya Arrizabalaga hataweza kuingia.

Sarri alionekana akipiga kelele za hasira pamoja na kupiga vitu kadhaa, akiangalia ubao wa magoli ukionesha 0-0, huku akiamini Arrizabalaga asingekuwa bora zaidi wakati wa mikwaju ya penati.

Ingawa alifanikiwa kuokoa mkwaju mmoja wa Leroy Sane, alijikuta akiachia mkwaju dhaifu kutoka kwa Sergio Aguero ukimpita chini yake.

Kocha Sarri amekielezea kitendo hicho kama ‘kutofautiana’, na amekiri kuwa hakufurahishwa na tabia ya golikipa huyo. Ameeleza kuwa anapanga kukaa naye chini ili wazungumze kiundani wiki hii.

“Alikuwa sahihi lakini kupitia njia isiyo sahihi. Kepa alitaka kunieleza kuwa yuko ‘fiti’ kuendelea na mikwaju ya penati. Lakini nitazungumza naye, nitamueleza kuwa anapaswa kuelewa kwamba anaweza kuingia kwenye matatizo hasa na nyie [waandishi wa habari],” alisema Sarri.

Naye nahodha wa zamani wa Chelsea, John Terry amesema kuwa kitendo alichokifanya goli kiga huyo ni utovu wa nidhamu kwa kocha.

“Umri wako unapozidi kuwa mkubwa unapaswa kurudi chini na kuonesha heshima. [Kama haukubaliani na uamuzi] utashughulika nayo baadaye, hivyo ndivyo mchezaji anapaswa kuwa,” Terry ameiambia Sky Sports.

Manchester City iliitandika Chelsea 4-3 kupitia mikwaju ya penati.

Mimba zakatisha masomo wanafunzi 57 Hai, Serikali yatangaza msako mkali
Treni yenye silaha nzito yampeleka Kim Jong Un kukutana na Trump

Comments

comments