Aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi wa Young Africans,  Abdul Sauko amewatahadharisha mashabiki wa Simba SC, kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Ahly utakaopigwa baadae hii leo.

Sauko ambaye pia aliwahi kuhudumu kama kongozi wa klabu ya Moro United iliyowahi kushiriki Ligi kuu Tanzania Bara, amesema mashabiki wa Simba SC wasitembee na matokeo mkononi, na badala yake wajipange kuishangilia timu yao kwa wakati wote.

Amesema mashabiki wa klabu hiyo wanapaswa kuamini soka lina matokeo ya kushangaza, kama ilivyokua kwa Simba SC walivyofanya mjini Kinshasa kwa kuifunga AS Vita Club kwenye uwanja wao wa nyumbani.

“Sina maana kwamba Simba ipo vibaya, ila mchezo wa soka una matokeo ya ajabu unaweza ukapata usichokitarajia kama kilichowakuta AS Vita Club kupigwa nyumbani kwao, mashabiki wao walijiamini kupitiliza, ndicho ninachowashauri mashabiki na wachezaji wa Simba kujituma kwa bidii,” amesema Sauko

Katika hatua nyingine Abdul Sauko amewataka wadau wa michezo nchini kuonesha ushirikiano kwa viongozi na wachezaji wa klabu za Simba SC na Namungo FC ambazo zina jukumu la kuiwaklisha nchi kmataifa msimu huu.

Amesema klabu hizo zinapaswa kuungwa mkono kuhakikisha zinafanikiwa kufika mbali zaidi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho.

“Ni kweli kuna ushabiki wa ndani lakini hizo timu kwasasa zinaiwakilisha Tanzania ukweli huo hautafutika, hivyo zipewe ushirikiano kama hivi tunavyoishauri Simba kuwa waangalifu katika mchezo wa kesho,” amesema.

Simba SC tayari imeshatinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na leo inacheza mchezo wa pili wa hatua hiyo dhidi ya Al Ahly, huku Namungo FC ikitanguliza mguu mmoja hatua ya makundi Kombe la Shirikisho kwa kuifunga Clube Desportivo 1º de Agosto ya Angola mabao 2-6 katika mchezo wa mkondo wa kwanza hatua ya 32 ya michuano hiyo. Mchezo wa mkondo wa pili kwa timu hizo utachezwa juma hili na mshindi wa jumla atatinga moja kwa moja hatua ya makundi Kombe la Shirikisho.

Manara amtuhumu Senzo Mazingiza
Balozi wa Italia nchini Congo auawa