Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ameupongeza uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure iliyoko jijini Mwanza kwa kuanzisha makambi ya huduma za kibingwa za uchunguzi bila malipo.

Prof. Makubi ametoa pongezi hizo wakati alipotembelea katika Hospitali hiyo kwa lengo la kuangalia namna huduma za afya zinavyotolewa sambamba na maboresho ya huduma za uchunguzi, ujenzi wa sehemu ya kufua hewa ya oksijeni na kuangalia maendeleo ya jengo la mama na mtoto pamoja na utekelezaji wa miradi ya fedha za IMF.

Aidha Prof. Makubi ametoa wito kwa vituo vya afya nchini kuanzia Hospitali za ngazi ya taifa hadi wilaya kuwa na utaratibu wa kuweka kambi za bure kwa wananchi walau kila baada ya miezi miwili kwa ajili ya uchunguzi wa kibingwa wa magonjwa hasa yasiyokua ya kuambukiza na kuwasisitiza wananchi kujitokeza kupima afya zao.

Kuhusu fedha za IMF Prof. Makubi amesema Hospitali ya Sekoue Toure imetengewa zaidi ya shilingi bilioni 1.9 kwa ajili ya vifaa vitakavyonunuliwa na kufungwa katika jengo la mama na mtoto ambalo linatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 22 mwaka huu na kuanza kutoa huduma kabla mwaka huu 2021 haujaisha.

Aidha, Prof Makubi ameendelea kusisitiza viongozi wote wa vituo vya afya nchini kusimamia vyema matumizi ya fedha katika ujenzi na ununuzi wa vifaa kwa kushindanisha wazabuni na wakandarasi ili thamani ya fedha iweze kuonekana huku akitoa miezi saba kuanzia tarehe 22 Novemba mwaka huu miradi yote iwe imeanza na kukamilika hadi kufikia tarehe 30 June mwaka 2022.

Breaking News: Soko la Manzese Tunduma laungua
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 16, 2021