Serikali imekamilisha zoezi la kupanga bei elekezi katika sekta ya afya ili kuwapunguzia wananchi mzigo wa gharama za huduma ya afya hususan katika hospitali binafsi.

Naibu waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, watoto na wazee, Dk. Khamisi Kigwangalla amewaambia waandishi wa habari kuwa bei hizo zitaanza kutumika hivi karibuni kwakuwa zmeidhinishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Dk. Kigwangalla aliyasema hayo hivi karibuni, muda mfupi baada ya kuzindua matokeo ya utafiti wa tathmini ya utoaji huduma za afya nchini wa mwaka 2014/2015.

“Bei elekezi zitaanza hivi karibuni lakini baadhi ya vituo tayari vimeanza kuvitumia kwa sababu tayari zimeshasainiwa na Waziri Mkuu,” alisema Dk. Kigwangalla. “Sasa hivi tunasubiri baraka za Waziri Mkuu ili tuzitangaze,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo alieleza kuwa serikali imepanga kupunguza idadi ya wagonjwa katika Hospitali ya Taifa ya Ikulu ambapo wagonjwa watakaokuwa wanatibiwa katika hospitali hiyo watakuwa wale walioandikiwa rufaa na hospitali za ngazi ya chini kwa ajili ya kupata huduma za madaktari bingwa.

Alisema kuwa Serikali itaongeza vikwazo vya kutibiwa katika hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na utaratibu utakaoelekeza mgonjwa kupata matibabu akitokea hospitali za ngazi za chini ambapo atahitaji kuwa na maelezo ya daktari anayepaswa kumuona pamoja na idhini kutoka kwa daktari husika.

“Hilo litakuwa suluhisho la kudumu la kuondoa msongamano katika Hospitali ya Muhimbili. Leo hii tumeongeza vitanda lakini wateja nao wameongezeka, nakuhakikishia baada ya miezi miwili utakuta wagonjwa wanalala chini tena,” Dk. Kigwangalla akakaririwa.

Ili kufanikisha dhamira hiyo, Naibu Waziri huyo alisema kuwa Serikali itaboresha hospitali za ngazi za chini ili wananchi wasione mapungufu ya huduma wazitakazo isipokuwa kwa wagonjwa watakaokuwa wanahitaji huduma za kibingwa ambao watalazimika kufika Muhimbili.

Mahakama yasema haya kuhusu kesi ya Kafulila, Mwilima
Timu ya Donald Trump yaendelea kumshambulia Papa Francis, yaja na zito zaidi