Klabu ya Leicester City ya Uingereza imeshindwa kukamilisha taratibu za usajili wa kiungo wa kati Adrien Silva kutoka katika klabu ya Sporting Lisbon baada ya kuchelewa sekunde 14 kuwasilisha makablasha ya usajili huo kwa Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA.

Leicester City walimnunua Adrien Silva kutoka Sporting Lisbon kwa ada ya pauni milioni 22 lakini walikamilisha mkataba huo karibu sana na wakati wa kufungwa kwa dirisha la usajili wa wachezaji tarehe 31 Agosti.

FIFA wamelikataa ombi la Leicester City kukamilisha usajili huo na hii ina maana kwamba mchezaji huyo ni wa Leicester lakini hawezi kuichezea timu hiyo mpaka pale dirisha la usajili litakapofunguliwa tena mwezi Januari.

Hata hivyo rais wa klabu ya Sporting Lisbon,  Bruno de Carvalho naye pia anaamini kuwa usajili wa Silva umekamilika lakini Leicester watatakiwa kusubiri mpaka mwezi Januari.

”Ningependa watu wajue kwamba FIFA haijakataa uhamisho wa Adrin, usajili umekamilika isipokuwa uandikishwaji wa mchezaji huyo natumaini mambo yatakuwa sawa na Leicester watampata mchezaji wao” alisema Bruno de Calvalho.

Silva ana umri wa miaka 28 ni mzaliwa wa Ufaransa na amekulia kwenye akademi ya klabu ya Sporting Lisbon

Leicester walimsajili kiungo Adriev ili kuziba pengo baada ya kumuuza kiungo wa kati Danny Drinkwater kwenda Chelsea kwa Pauni milioni 35 kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Alhamisi wiki iliyopita.

 

 

Wilaya ya Sikonge kuanzisha zao la Korosho
RC Tabora aagiza kukamatwa kwa viongozi wa ushirika