Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, amemtahadharisha Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro kwamba wananchi wa jimbo lake hawajasahau tukio la Msaidizi wa Mbowe aliyepotelea kusikojulikana kwani bado wana hasira inayofukuta moyoni.

Amesema kuwa yeye kama Mbunge wa Rombo na Ben Saanane akiwa ni mpiga kura wake analitaka jeshi la polisi pamoja serikali waweze kutoa ripoti ya kijana huyo kama bado yupo hai au ameshafariki ili wafanye matanga vinginevyo wao wataamua wenyewe cha kufanya.

“Nataka nimwambie IGP  Sirro na Watanzania wote kwa ujumla ipo siku warombo tutaitana kufanya maamuzi, nataka niwaambie warombo damu ya mwenzetu haiwezi kupotea Halafu sisi tukakendelea kukaa kimya kama wajinga, Lazima tufanye maamuzi sahihi. Vijana wa Rombo popote pale mlipo nataka kuwaambia mwaka huu hautaisha lazima tukutane tuamue juu ya mwenzetu,”amesema Selasini

Aidha, Mbunge huyo amesema kuwa familia ya Ben Saanane imekuwa na huzuni tangu kupotea kwa kijana wao ambapo mpaka sasa jeshi la polisi halijawahi kutoa ripoti tangu taarifa za kupotea kwake zilipotangazwa.

Hata hivyo, Ben Saanane ambaye alikuwa Msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, tangu kuripotiwa kupotea kwake ni takribani mwaka sasa ambapo si familia, jeshi la polisi au Chama chake wanajua ni wapi alipopotelea huku chama chake kikiendelea kuliomba jeshi la polisi na serikali kufanya uchunguzi kuhakikisha anapatikana

Video: Makamba, Nchemba, Mwakyembe, wapeta baraza jipya la mawaziri
Trump kuitosa Iran mkataba wa nyuklia