Serengeti Boys inayokwenda kuweka kambi huko Antananarivo, Madagascar inatarajiwa kufika huko saa 8.10 mchana. Timu hiyo inajiandaa kucheza na Afrika Kusini katika mchezo wa awali kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika utakaofanyika Agosti 6, 2016.

Mchezo wa marudiano utafanyika Agosti 21, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam. Serengeti ipo kwenye ushindani wa kuwania nafasi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana, zitakazofanyika mwakani huko Madagascar.

Wakati mkuu wa msafara akiwa ni Ayoub Shaibu Nyenzi ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Vijana, maofisa wengine waliosafiri na timu hiyo ni Kocha Mkuu, Bakari Nyundo Shime, Daktari wa timu hiyo, Shecky Francis Mngazija na Mtunza Vifaa, Andrew Vanance Andrew pamoja na Juma Kaseja Juma ambaye kwa muda amechukua nafasi ya makocha wasaidizi, Sebastian Nkoma na Muharam Mohammed ‘Shilton’ wanaohudhuria kozi ya makocha ngazi ya juu inayoratibiwa na CAF.

Nyota waliosafiri ni pamoja na makipa, Ramadhani Awm Kabwili, Kelvin Deogratius Kayego na Samwel Edward Brazio wakati mabeki wako Kibwana Ally Shomari, Nickson Clement Kibabage, Israel Patrick Mwenda, Dickson Nickson Job, Ally Hussein Msengi, Issa Abdi Makamba na Enrick Vitalis Nkosi.

Viungo ni Kelvin Nashon Naftal, Ally Hamisi Ng’anzi, Asadi Ali Juma Ali, Syprian Benedictor Mtesigwa, Ibrahim Abdallah Ali, Shaban Zuberi Ada huku washambuliaji wakiwa ni Mohammed Abdallah Rashid, Yohana Oscar Mkomola na Muhsin Malima Makame.

“Najua mchezo utakuwa mgumu, lakini nakiamini kikosi change. Kiko imara,” amesema Shime, maarufu zaidi kwa jina la Mchawi Mweusi.

Serengeti Boys inakwenda kucheza na Afrika Kusini baada ya kuwatoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0 katika mechi zake mbili za kimataifa. Mshindi wa jumla kati ya Serengeti Boys na Afrika Kusini, atacheza na timu mshindi kati ya Namibia na Congo-Brazaville.

Hivi karibuni Serengeti Boys ilifanya ziara India ambako walishiriki mashindano ya vijana ya Kimataifa yanayotambuliwa na FIFA (AIFF International Youth Tournament 2016) kabla ya kurudi na rekodi ya kupigiwa mfano si tu katika Tanzania na kwa nchi za Afrika Mashariki. Ilishika nafasi ya tutu nyuma ya Korea Kusini na Marekani.

 

Padri auawa akiendesha ibada kanisani
TCU Yakanusha Taarifa za Kuvifungia Udahili wa Kozi Tofauti Vyuo 22