Timu ya soka ya Taifa ya Vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ leo Mei 19, 2016 imetinga hatua ya Nusu Fainali baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Korea Kusini katika mfululizo wa michuano maalumu ya kimataifa yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIF Youth Cup 2016 U-16).

Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Tilak, Maidan mjini Goa, India mabao ya Serengeti yalifungwa na Assad Juma katika dakika ya 12 na Maulid Lembe katika dakika ya 87 ambaye alisawazisha baada ya Korea kutangulia kwa mabao 2-1.

Matokeo hayo yanaifanya Serengeti Boys ifikishe pointi tano na kwamba inasubiri matokeo ya mwisho kati ya Korea Kusini na Marekani yatakayotoa mwanga wa timu itakayocheza fainali.

Kadhalika matokeo hayo, yamewafurahisha Watanzania, lakini zaidi Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu ya Airtel Tanzania, Jackson Mbando aliyepongeza mafanikio ya Serengeti Boys inayoundwa na nyota wengi kutoka katika mradi wa kuibuka na kukuza vipaji unaodhaminiwa na Kampuni ya simu za mkononi ya Airtel maarufu kama Airtel Rising Stars (ARS).

Mbando alitoa pongezi hizi Mei 18, 2016 alipokutana na Sekretarieti ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambako pamoja na mambo mengine walijadili namna ya kuendeleza mradi huo ambao kwa sasa theluthi moja ya wachezaji wa Serengeti Boys iliyoko India kushiriki michuano maalumu ya kimataifa yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka nchini humo (AIF Youth Cup 2016 U-16), wanatoka ARS.

Mbando alitoa pongezi hizo wakati Serengeti Boys inaingia tena Uwanja wa Tilak, Maidan mjini Goa, India kuivaa Korea Kusini katika mfululizo wa mechi hizo huku akisifu juhudi za Mohammed Abdallah aliyeisawazishia Serengeti Boys katika mchezo dhidi ya Marekani uliofanyika Jumapili Mei 15, mwaka huu katika dakika ya 16. Katika mchezo huo ulioshia kwa sare ya 1-1dhidi ya Marekani, Jean Jullien alianza kuifungia timu yake katika dakika ya 5.

Kadhalika nyota wa Airtel Rising Stars waling’ara tena katika mchezo wa Mei 17, 2016 kuwasambaratisha wenyeji India kwa mabao 3-1. Katika mchezo huo mbali ya Abdallah nyota wengine wa Airtel Rising Stars wanaong’ara India Maziku Amani aliyefunga bao la kwanza katika dakika ya 21, pia Nickson Kibabage aliyepiga krosi iliyowachanganya mabeki wa India na kufunga bao katika dakika ya 28 kabla ya Asad Juma kutungua la tatu katika dakika ya 48. Bao la India lilifungwa na Komal Thatal ( dakika ya 38).

Wengine wanaotikisa India ni Ally Msengi, Nickson Job, Ally Ng’anzi na Syprian Mwetesigwa ambako kwa mujibu wa taarifa kutoka Idara ya Ufundi ya TFF, msingi wa nyota hao na wengine ni wale waliokuzwa kutoka mashindano ya Coca-cola.

Mbali ya mchezo wa leo, pia nyota wa timu hiyo ya Serengeti Boys watashuka dimbani tena Mei 19, 2016 watamaliza dhidi ya Malaysia Mei 21, 2016. Fainali ya michuano hiyo itachezwa Mei 25, 2016 na kabla ya mchezo wa fainali, utachezwa mchezo wa mshindi wa tatu katika uwanja huo huo Tilak Maidan, Vasco, Goa nchini India.

India kimeandaa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 17, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kikosi chao kwa ajili ya Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana zitakazofanyika nchini humo mwaka 2017.

Hivi Ndivyo Azam FC Walivyopoteza Point Tatu Za Ligi Kuu
TFF Wachimba Mkwara Mzito Kuelekea Michezo Ya Mwisho Ya Ligi

Comments

comments