Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itahakikisha inalinda amani ya nchi kwa gharama zozote na kamwe haitoruhusu mwanasiasa yeyote kusababisha vurugu zitakazochochea uvunjifu wa amani.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na viongozi wa dini pamoja na wazee wa mkoa wa Rukwa mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.

Majaliwa amesisitiza kuwa – “Hatuzuii kuwa na vyama vya siasa ila haturuhusu vurugu kupitia vyama vya siasa na hakuna jambo lisilokuwa na mipaka. Mambo ya kuhamasishana kufanya vurugu hatutayaruhusu, tunataka watu wafanye kazi,”

Amesema Serikali inataka Watanzania wawe na uhakika wa kuendelea kufanya kazi zao za kuwaingizia kipato na kuwaletea tija, hivyo suala la kudumisha amani ni muhimu kwani vurugu zikitokea hawatakuwa na mahali pa kukimbilia na hakuna shughuli ya maendeleo itakayofanyika.

Pia, Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake kwa sababu kazi ya uongozi ni ngumu na inachangamoto nyingi.Pia aliwaagiza viongozi wa dini wa mkoa wa Rukwa kuharakisha uundwaji wa Kamati ya Amani ya mkoa huo.

Kwa upande wa Sheikh wa mkoa wa Rukwa, Sheikh Rashid Akilimali amesema madhehebu ya dini hayawezi kuvuruga amani ya nchi ila anahofu na viongozi wa vyama vya siasa kutokana na vitendo vyao vya kuhamasisha vurugu.

Sheikh Akilimali aliwaomba wanasiasa nchini kutovuruga amani kwani machafuko yakitokea watashindwa kufanya ibada mbalimbali ikiwemo kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Tafadhalini wanasiasa msituharibie amani ya nchi yetu. Amani haichezewi tunaona kwa wenzetu wanavyohangaika, wanaishi kwa tabu sisi hatujazoea  kukimbia. Sisi Watanzania ni moja na tunaishi kwenye nyumba moja hivyo hatuna budi kushirikiana kuilinda amani yetu,” alisema.

Na Katibu wa Wazee mkoani Rukwa, Kanali Mstaafu, John Mzurikwao alimuomba kiongozi huyo kuwasaidia  kutatua kero mbalimbali zinazoukabili mkoa huo zikiwemo za malipo ya pembejeo kwa mawakala wa kilimo pamoja na mgogoro wa ardhi katika shamba ya Efatha.

Waziri Mkuu alisema suala la malipo kwa mawakala wa pembejeo za kilimo linafanyiwa kazi na watalipwa baada ya Serikali kukamisha zoezi la uhakiki wa madeni hayo ili kujiridhisha kama kweli wakulima wapatiwa pembejeo na kwa kiwango gani.

Majaliwa;Atakayevamia Misitu Faini millioni 70, Au Jela Miaka Saba
Video: Makonda apokea vifaa vya usafi vyenye thamani ya milioni 10 kutoka AAR Isurance