Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imetoa tahadhari ya mlipuko wa Virusi vya Corona na kusema wamekuwa wakifuatilia mlipuko huo tangu ulipoanza Nchini China na kusambaa katika mataifa mengine.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Afya imesema, hakuna muathirika wa Virusi vya Corona nchini Tanzania. Hata hivyo imeweka wazi kuwa, kutokana na Mahusiano ya Kijamii na Kibiashara yaliyopo kati ya Tanzania na Bara la Asia, kuna hatari kuwa Virusi hivyo vinaweza kuingia nchini.

Serikali imetoa tahadhari wa Watanzania wanaosafiri kuelekea China, pamoja na Thailand, Japan, Marekani na Korea Kusini ambazo zimeripoti maambukizi hayo. Tahadhari pia imetolewa kwa wanaopokea wageni kutoka nchi hizo.

Tayari watu 830 wameshaambukizwa kirusi hicho, huku 26 wakipoteza maisha na mamilioni wengine wamewekwa chini ya karantini katika juhudi za kujaribu kudhibiti kusambaa kwake.

Taasisi inayoshughulikia chanjo na kinga za maradhi duniani imesema, chanjo dhidi ya kirusi hicho inaweza kupatikana katika kipindi cha mwaka mmoja unaokuja.

 

Wakuu wa EU watia saini makubaliano ya Brexit
Magufuli aruhusu makontena ya Makinikia yaliyozuiwa 2017 yauzwe