Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaofanywa na Taasisi pamoja na vituo vya kukuza vipaji katika sekta ya michezo hapa nchini kwakua imechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa wachezaji wengi walioliwakilisha Taifa vizuri katika mashindano mbalimbali.

Ameyasema hayo Jijini Dododma alipotembelea kituo cha mafunzo ya Michezo cha Foutain Gate Academy ambapo mbali na kuupongeza uongozi wa kituo hicho na kuahidi kutafuta wafadhili mbalimbali watakaowezesha kituo hicho kufanya vizuri zaidi.

”Mnafanya kazi kubwa sana ya kuibua na kukuza vipaji, nawaahidi Serikali itaendelea kushirikiana nanyi pale ambapo mtakwama ikiwemo kutuma timu ya Wataalam wa michezo kutoka Wizarani ili waje kutoa ushauri wa kitaalam katika michezo pamoja na kupokea maoni kutoka kwenu ili kwa pamoja tukuze sekta ya michezo,” amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha, Dkt.Mwakyembe ameiagiza Idara ya Maendeleo ya Michezo kufika katika kituo hicho kuona namna mafunzo yanavyoendeshwa pamoja na kutoa elimu kuhusu taaluma za Michezo zinazotolewa na Chuo cha Michezo cha Malya ili wakufunzi wa kituo hicho waweze kwenda kujifunza zaidi katika chuo hicho.

Naye Mkuu wa Shule ya Sekondari hiyo, Dennis Joel amesema kuwa shule hiyo mbali na kutoa elimu imeweka Michezo kipaumbele ili kupata vijana wengi wasomi lakini pia wanaoweza kucheza michezo mbalimbali ambayo inaweza kuwapatia ajira.

Kwa upande wake Meneja wa Kituo hicho, Wendo Makau amesema kituo hicho kinalengo la kukuza vipaji na kuwaandaa vijana watakaoshiriki michezo nje ya nchi kwakua vijana wengi wana ndoto ya kufikia hatua ya kucheza nje ya nchi.

Naye Nahodha wa timu ya mpira wa miguu chini ya umri wa miaka 20 Ramadhan Albert amesema anashukuru nafasi aliyopata ya kujiunga na kituo hicho kwakua ndoto zake ni kuwa mwanamichezo mkubwa ndani na nje ya nchi.

Sababu ya kasi ya ugonjwa wa TB nchini yawekwa wazi
Video: Jua halinichoshi, Naamka alfajiri | Mama anayezungusha mboga Mtaani kwenye beseni