Serikali ya Kenya imeweka amri ya kutotoka nje usiku kwa siku 30 katika eneo la pwani la Lamu, kufuatia mauaji ya watu saba, wawili kati yao walikatwa vichwa na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kiislamu.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi amesema amri hiyo ya kutotoka nje inalenga kusaidia vikosi vya usalama kuwatafuta wanamgambo hao na hadi sasa washukiwa kadhaa tayari wamekamatwa, kwa mujibu wa msemaji wa polisi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo maeneo yatakayoathiriwa na kafiu hiyo ni pamoja na: Mukunumbi, Majembeni, Ndamwe, Mkunumbi, Witu, Pandanguo, Binde Warinde, Hamasi, Mpeketoni, Bomani, Pongwe, Mpeketoni, Bahari, Mapenya na Lamu Central.

Hali ya wasiwasi inazidi kushuhudiwa katika eneo hilo ambalo limekuwa likishambuliwa mara kwa mara.

Seneta wa Lamu Anwar Loitiptip amekuwa kiongozi wa wa mwanzo kukashifu vikali mauaji ya kinyama ya watu hao yalitokelezwa kwenye kijiji cha Widhu-Majembeni katika Kaunti ya Lamu.

Aidha ameitaka serikali kuu kupitia idara ya usalama kufuatilia kwa makini matukio hayo na kuhakikisha wote waliohusika wanakamatwa na kukabiliwa kisheria.

Hata hivyo kitendawili cha mauaji hayo yaliyotekelezwa Januari 3, 2022, bado hakijateguliwa kwani yapo madai kwamba kundi gaidi la Al Shabaab lilihusika huku madai mengine yakiwa ni kuhusu mzozo wa ardhi.

Wapiganaji wa Al-Shabaab wamefanya mashambulizi kadhaa makubwa ndani ya Kenya kulipiza kisasi kutokana na serikali ya nchi hiyo kuwapeleka wanajeshi wake nchini Somalia mwaka 2011 kama sehemu ya kikosi cha Umoja wa Afrika.

Kundi hilo linaloshirikiana na mtandao wa Al Qaeda linataka kuiondoa madarakani serikali ya mjini Mogadishu inayoungwa mkono kimataifa.

Burna Boy ajizawadia Gari la kifahari
Volkano ya Nyiragongo DRC yalipuka