Serikali imesema kuwa Shirika la Ndege nchini (ATCL), litaendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha inaboresha huduma za usafiri wa anga katika visiwa vya Unguja na Pemba.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano , Mhandisi Edwin Ngonyani katika kikao kilichokutanisha Baraza la Waakilishi la Kamati ya Mawasiliano na Ardhi kutoka Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na uongozi wa Shirika hilo.

“Nawahakikishia wajumbe wa kamati hii kuwa changamoto mlizonazo tutazifanyia kazi haraka kwani ATCL sasa imezaliwa upya na hivyo itahakikisha inaboresha maslahi ya kuliinua na kuliendeleza shirika ili kuweza kukidhi mahitaji ya hapa na visiwani”, amesema Naibu Waziri Ngonyani.

Aidha, Mhandisi Ngonyani ameongeza kuwa katika kuhakikisha huduma za usafiri wa anga visiwani humo zinaimarika, tayari Serikali imeshaanza kulipa deni lililokuwa linadaiwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege la shilingi milioni 241 ambalo shirika hilo linadaiwa kutokana na tozo ya maegesho ya ndege na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hamza Juma amemwomba Naibu Waziri Mhandisi Ngonyani kuangalia upya suala la ajira katika Shirika la ATCL ili liweze kubeba sura ya Muungano na kuwawezesha wataalam wenye sifa kutoka Zanzibar nao kupata nafasi hizo.

 

Video: Manji anatumia 'unga' - Mkemia Mkuu, Bombardier yamtia Lissu matatani
Bombadier yamkaanga Lissu, alala rumande