Serikali nchini, imeanza kuboresha mashamba yake ya mifugo, kwa kununua ng’ombe ili kuongeza uzalishaji na kuuza kwa watu binafsi na kwamba inatarajia kuzindua ugawaji wa Mitamba (Ng’ombe jike ambao bado hawajazaa), katika Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma na Wilaya nyingine zaidi ya kumi ili iende kwa watu hao na vikundi vya wafugaji.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameyasema hayo wakati akikabidhi Ng’ombe 1,160 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.9 iliyofanyika katika Shamba la Kuzalisha Mifugo la Mabuki Wilayani Misungwi Mkoani Mwanza, lililopewa Ng’ombe 500, Shamba la Sao Hill la Mkoani Iringa, ng’ombe 500 na Shamba la Kitulo la Mkoani Mbeya, ng’ombe 160.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (wanne kushoto), akikata utepe kuashiria kupokea Ng’ombe jike 1,160 wenye thamani ya Shilingi Bilioni 2.9 katika hafla fupi iliyofanyika kwenye Shamba la Kuzalisha Mifugo la Mabuki lililopo Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza.

Amesema, lengo la kugawa Mitamba hao ni kuhakikisha wafugaji wanapata mifugo itakayokuwa na tija ili kupata nyama ya kutosha pamoja na maziwa na kwamba kutakuwa na kampeni ya kuhamasisha wafugaji kupandikiza mifugo yao mimba kwa njia ya chupa (uhimilishaji), ili kupata matokeo bora ya mifugo itakayozaliwa kwa kutumia mbegu bora.

Waziri Ndaki ameongeza kuwa, “Tutaendelea kugawa mitamba katika bajeti zijazo ili mashamba yetu yote ya serikali yaweze kuwa na mitamba inayotosha ili wafugaji wetu wakitaka kuchukua ili wakabadilishe aina ya ngo’mbe tunayofuga Tanzania waweze kupata kiurahisi na tunamshukuru pia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanya mageuzi kwenye sekta ya Mifugo.”

Msimu wa Utamaduni SA na Tanzania umewadia
Mifumo ufahamu wa Takwimu kuimarishwa: Dkt. Katunzi