Serikali nchini, imesema itaendelea kutekeleza miradi muhimu ya huduma za kijamii, ikiwemo maji, elimu na afya ili kupunguza adha zinazowakabili wananchi na kuwasaidia kupata maendeleo.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ameyasema hayo wakati akizindua mradi wa maji katika Kijiji cha Sibwesa kilichopo Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi, uliogharimu shilingi milioni 173.2.

Katika hatua nyingine, akiwa Kijijini hapo pia Makamu wa Raisameagiza kupelekwa kwa mtaalamu wa Kilimo katika Kijiji hicho, ili kuwasaidia wananchi kufanya kilimo cha kisasa na kuongeza uwingi wa upatikanaji wa mazao.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango amezindua mradi wa maji wa Sibwesa uliopo Wilayani Tanganyika Mkoani Katavi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maji, Maryprisca Mahundi amesema sera ya Wizara ya Maji ni kuhakikisha huduma hiyo, inafikishwa katika taasisi zote za Kiserikali na za Kiraia.

Amesema, “pamoja na uwepo wa mradi huo pia Serikali inatarajia kutekeleza mradi wa shilingi bilioni 1.8 ili kuisaidia Wilaya hii katika vijiji vinne vya vya Nkungwi, Kasekese, kaseganyama na Sibwese kufikiwa na huduma.”

Naye, Mbunge wa Mpanda Vijijini, Selemani Kakoso ameipongeza serikali kwa kutekeleza mradi huo ambao umepelekea mabadiliko, katika Kijiji hapo na kuwawezesha wanafunzi kutumia kikamilifu muda wa masomo tofauti na awali.

Wananchi wakienda kuchota maji katika moja ya maeneo, nchini Tanzania.

Amesema, wanafunzi hao walikuwa wakitafuta huduma ya maji muda mwingi na kuiomba serikali kuisaidia Wilaya ya Tanganyika na Mkoa wa Katavi, kuondokana na changamoto ya maji kwa kutumia ziwa Tanganyika ambalo ni chanzo cha uhakika.

Mradi huo, umewezesha kupatikana kwa maji safi na salama katika taasisi zote zilizopo eneo la Sibwesa pamoja na kuwasaidia wananchi kuondokana na maradhi yaliyokuwa yakitokana na utumiaji wa maji yasiyo safi na salama, hapo awali.

Waziri 'afagilia' utendaji wa TANAPA
Serikali yawaasa Vijana kuthamini vipaji