Serikali imesema kuwa inafanya marekebisho ya tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara wakiwemo wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kupata pembejeo na kuzipeleka mpaka ngazi za Vijiji.

Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama juu ya mpango wa Serikali katika kupunguza tozo za maduka yanayouza pembejeo ili kuwawezesha wakulima kupata pembejeo hizo hata katika ngazi ya Vijiji na kwa gharama nafuu.

“Ni kweli kwamba Serikali imepokea ushauri na malalamiko kadhaa kutoka kwa Wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa maduka ya pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima za biashara,” amesema Majaliwa.

Aidha, amesema kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Serikali sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote ambapo mawaziri wenye dhamana ambao wanatozo mbalimbali kwenye wizara zao zinazokwamisha kufanya biashara katika mazingira rahisi wameshakutana ili kuangalia tozo zinazohitaji kupitiwa upya.

“Kwa sasa mkakati wa Serikali unaendelea na niwape matumaini wafanyabiashara wote nchini kwamba Serikali imesikia vilio vyao, na tunafanya mapitio ya tozo hizo na tutakapofikia hatua nzuri  tutawajulisha ili kujua ni aina gani ya tozo tunataka tuiondoe au kuibadilisha ili muendelee kufanya biashara zenu kwa mazingira rahisi,’’ amesema Waziri Mkuu.

Video: Sababu yatajwa ugonjwa wa Dengue kutibiwa na maji na Panadol
Uchaguzi Malawi: Mutharika apigwa chini Urais na Upinzani