Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamilia kumaliza changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini ambapo imetenga zaidi ya sh. trilioni moja kwa ajili ya kumalizia kazi ya usambazaji umeme nchi nzima ikiwemo wilaya ya Mlele.

Majaliwa amesema watapeleka jenereta kubwa mbili zitakazofungwa katika kijiji cha Utende ambazo zitasambaza na kuwasha umeme katika kata ya Inyonga na maeneo mengine.

“Mwezi Novemba mwaka huu umeme utakuwa umewaka wilayani Mlele. Mkakati ni kuunganisha mkoa wa Katavi na gridi ya Taifa kutoka Tabora, kupita Sikonge hadi Inyonga,“ – Majaliwa.

Aidha, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji na mbunge wa jimbo la Katavi, Mhandisi Isack Kamwelwe amemuomba Waziri Mkuu kuwasaidia kupandishwa hadhi kwa kituo cha afya cha Inyonga na kuwa Hospitali ya wilaya kwa sababu wilaya yao haina hospitali.

Pia ameomba wilaya hiyo ipatiwe umeme wa Tanesco ili kupunguza gharama kubwa za kununua umeme kutoka kwa mfanyabiashara ambaye amefunga jenereta na anawauzia unit moja sh. 1000 wakati Tanesco wanauza sh. 100 kwa unit moja.

Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Mlele, Rachel Kassanda alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa nyumba za watumishi hali inayosababisha mkuu wa wilaya na Katibu tawala wa wilaya kuishi kwenye nyumba za kupanga.

Picha: Majaliwa akutana na Waziri mkuu mstaafu, Pinda wilayani Mlele
Mabomu ya Machozi yaiamsha Moshi