Serikali imeahidi kuhifadhi kumbukumbu na takwimu sahihi za urithi wa Utamaduni usioshikika kwa lengo la kuuendeleza na kuiwezesha jamii kuulinda kwa ajili ya vizazi vijavyo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel alipokua akifungua warsha ya siku kumi iliyoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kuhusu urithi wa Utamaduni Usioshikika leo Jijini Dar es Salaam.
Aidha, Prof. Gabriel amewataka washiriki kujifunza vizuri ili baadaye waweze kusaidia katika kuwekeza, kuibua, kutambua na kutunza urithi wa utamaduni usioshikika kwani hiyo ndio njia mojawapo itakayowavutia watalii wengi kuja nchini kujifunza tamaduni zetu zisizoshikika.
“Utamaduni ni nta inayowaweka watu pamoja, ni vyema mafunzo haya na utaalamu mtakayoipata izingatie kuibua fursa na kutambua tamaduni ambazo hazishikiki kwani serikali ina malengo na matumaini makubwa sana kutoka kwenu” alisema Prof. Gabriel.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Mathias Luhanya amesema kuwa dhumuni la warsha ni pamoja na kuwajengea uwezo wadau wa utamaduni namna ya kuhifadhi urithi wa utamaduni usioshikika ili baadaye waweze kuorodhesha urithi huo kwani Tanzania ina bahati ya kuwa na jamii zaidi ya 120 hivyo ni matarajio kuwa urithi wa utamaduni usioshikika umesheheni ndani ya kila jamii.