Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaweka mikakati madhubuti kwa lengo la kuimarisha matumizi ya fukwe kama sehemu ya kivutio cha utalii ili kongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini na kutengeneza ajira kwa wananchi.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati alipomwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye ufunguzi wa onyesho la Kimataifa la Utalii la Swahili International Tourism Expo, katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC).

Onyesho hilo linalofanyika kwa siku tatu nchini linahudhuriwa na wafanyabishara wakubwa wa utalii takribani 170  kutoka nchi mbalimbali duniani pamoja na wauzaji wa bidhaa za utalii takribani 300 kutoka ndani na nje ya nchi.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa sekta ya utalii nchini inachangia zaidi ya asilimia 25 ya mauzo yote ya nje na takribani ajira 1,500,000, ambapo kati ya ajira zote za moja kwa moja na zile ambazo si za moja kwa moja.

Pia ameongeza kuwa kutokana na juhudi za utangazaji wa vivutio vya utalii nchini unaoratibiwa na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), wageni wengi maarufu duniani wanakuja kuona vivutio hivyo wakijua kwamba Tanzania ni nchi ya amani, yenye utulivu na Watanzania ni watu wakarimu.

Hata hivyo, katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemshukuru Rais Dkt. John Magufuli kwa mchango wake mkubwa kwenye maendeleo ya sekta ya utalii nchini kutokana na hatua mbalimbali anazozichukua katika kukuza sekta hiyo.

 

Mbowe ajibu mapigo, adai Chadema ilishiriki msiba wa ajali ya MV. Nyerere
Riyama azamia kwenye muziki, 'Wimbo umetoka na unapendwa'