Serikali imeahidi kufanya kazi kwa karibu zaidi na vyombo vya habari huku ikiongeza kuwa inathamini na kutambua mchango mkubwa unaotolewa na Vyombo hivyo nchini katika kuhakikisha kuwa jamii inapata taarifa sahihi na kwa wakati.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Prof. Elisante Ole Gabriel alipotembelea vyombo vya habari vya Radio EFM/Radio One/ITV mapema hii leo jijini Dar es salaam, ambapo amesema kuwa lengo kubwa la Serikali ni kuwepo kwa ushirikiano mzuri na sekta ya habari nchini.

“Lengo la ziara hii ni kuimarisha uhusiano baina ya Serikali na vyombo vya habari pamoja na kufahamu utendaji wenu wa kazi na namna mnavyosimamia maudhui ya vipindi vyenu mnavyoviandaa” amesema Prof. Gabriel

Aidha amesema kuwa ni jambo jema linalofanywa na watanzania wazawa kuwekeza katika sekta ya habari kwa kuwa dunia ya sasa imetawaliwa na utandawazi kupitia taarifa mbalimbali zinazotolewa zenye lengo la kuhabarisha na kujenga taifa letu.

Vile vile, Prof. Gabriel amewataka watumishi wa vyombo vya habari kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa kujituma ili kupata matokeo chanya katika soko la ushindani na kuifikia jamii kubwa zaidi katika kutoa habari za uhakikia na zenye usahihi.

Hata hivyo, amevitaka vyombo vya habari kuzingatia maudhui yanayoendana na jamii ya kitanzania pale wanapoandaa vipindi mbalimbali ili kujenga jamii yenye utamaduni mzuri ikiwemo kufanya kazi kimkakati.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Radio One/ITV,  Joyce Mhaville ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Habari kwa kuonyesha ushirikiano mzuri na vyombo vya habari ikiwemo kufanya kazi kwa karibu na  kuviwezesha vyombo hivyo  kupata habari zenye ukweli na uhakika.

Video: Prof. Lipumba amnanga Maalim, ataka Bashange ashughulikiwe
NEC yafanya uteuzi wa wabunge nane wa viti maalumu CUF